CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amewasihi wananchi na wadau wa usafiri ardhini nchini kuzingatia matakwa ya Amri ya Miamala ya Kielektroniki (Malipo ya Lazima kwa Njia za Kielektroniki kwa Miamala Iliyoainishwa), 2026, iliyoanza kutumika rasmi tarehe 1 Julai 2026.
Dkt. Suluo amesema hayo Septemba 24, 2026, kwenye mkutano na wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam alipozungumzia mafanikio ya LATRA ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Suluo amesema Amri hiyo imetolewa na Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) Waziri wa Fedha chini ya kifungu cha 13(2) cha Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442, na inataka malipo yanayohusiana na miamala iliyoainishwa katika Jedwali la Amri hiyo kufanyika au kupokelewa kupitia njia za kielektroniki. Amesisitiza kuwa wadau wa usafiri ardhini wanapaswa kuisoma, kuielewa na kuzingatia matakwa yake katika shughuli zao za kila siku.
“Miamala ya usafiri ardhini inayohusika na matakwa hayo inajumuisha malipo ya ada, tozo na ushuru, pamoja na malipo ya nauli zinazohusiana na huduma za mabasi yaendayo haraka (BRT), vivuko, madaraja, mabasi ya abiria ya masafa marefu, teksi mtandao, usafiri wa reli na huduma za maegesho.”
Aidha, Dkt. Suluo amesema Amri hiyo inahusu pia miamala mingine iliyoorodheshwa, ikiwemo malipo yanayofanyika katika vituo vya kujaza mafuta, malazi, chakula na vinywaji katika hoteli, migahawa na mikahawa, huduma za utalii, pamoja na ununuzi na uuzaji wa magari. Amewataka watoa huduma na wananchi wanaohusika na miamala hiyo kuhakikisha wanatumia njia za kielektroni pale inapohitajika kwa mujibu wa Amri hiyo.
LATRA itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala yanayohusu usafiri ardhini ili kuhakikisha wadau wanafahamu wajibu wao na huduma zinaendelea kutolewa kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni zilizopo.

