JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA UDHIBITI USAFIRI ARDHINI
MRADI WA USAFIRI JUMUISHI NA ENDELEVU WA DODOMA
(DIST) – NAMBA YA MRADI: P176623
HADIDU ZA REJEA
KWA AJILI YA
HUDUMA ZA USHAURI WA KITAALAMU KWA MTAALAMU WA USAFIRI WA UMMA
Zabuni Na. AE.092/WBDIST/P176623/555181/2026/27/IC/01
NOVEMBA 2026
HADIDU ZA REJEA (TOR)
Kwa Mtaalamu wa Usafiri wa Umma (kumsaidia LATRA katika Mageuzi ya Uendeshaji wa Usafiri wa Umma (Daladala) katika Jiji la Dodoma).
1. Usuli
Dodoma, mji mkuu wa Tanzania, inakabiliwa na mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya ukuaji wa idadi ya watu katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (wastani wa asilimia 6.4 kwa mwaka), kufuatia kuharakishwa kwa uhamishaji wa shughuli za makao makuu ya taifa na Serikali. Ukuaji huu wa haraka wa miji umesababisha maendeleo ya makazi na shughuli za kiuchumi yaliyotawanyika katika maeneo mengi, na kuongeza kwa kiasi kikubwa umbali wa safari pamoja na mahitaji ya mfumo bora na endelevu wa usafiri wa umma. Kwa sasa, usafiri wa umma unatawaliwa na waendeshaji wa mabasi madogo (daladala), wakisaidiwa na teksi za magurudumu mawili na matatu. Mfumo huu uliogawanyika unaoendeshwa na waendeshaji binafsi unakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo ukusanyaji wa mapato unaotegemea malengo ya kila siku unaochochea uendeshaji wa hatari na ushindani wa kutafuta abiria. Hali hii husababisha muda wa kusubiri usiotabirika, uzoefu duni kwa abiria, na kupungua kwa1 sehemu ya matumizi ya mabasi madogo katika usafiri. Aidha, mfumo wa sasa wa biashara hauzingatii mahitaji ya upatikanaji wa huduma kwa watu wote, jambo linaloibua changamoto kubwa za usalama na ulinzi, hususan kwa wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, Serikali ya Tanzania, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usafiri Jumuishi na Endelevu wa Dodoma (DIST), inatekeleza mpango mpana wa kuboresha miundombinu na huduma za usafiri katika Jiji la Dodoma. Chini ya Kipengele Ndogo cha 1.2 cha mradi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inaongoza mageuzi muhimu ya usafiri wa umma. Mpango huu unalenga kuiwezesha LATRA kusimamia mabadiliko ya shughuli zisizo rasmi za daladala kuwa taasisi/kampuni rasmi za biashara zinazomilikiwa au kuendeshwa kwa pamoja.
Mageuzi haya yanalenga:
- kuwaunganisha waendeshaji katika vyombo rasmi vyenye muundo, kama vile vyama vya ushirika au kampuni;
- kuboresha ubora, usalama na uhakika wa huduma za usafiri wa umma;
- kupunguza msongamano wa magari na kiwango cha hewa ukaa kinachozalishwa; na
- kuandaa ujumuishaji wa huduma za daladala katika mfumo wa baadaye wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) au mifumo mingine yenye uwezo mkubwa wa kubeba abiria, kwa kuzingatia mpango wa jumla wa usafiri wa umma wa jiji.
1 Katika Dodoma kuna korido ambazo bodaboda ndiyo njia ya usafiri inayotumika zaidi. Hata hivyo, kuna korido ambazo daladala ndizo njia inayopendelewa, lakini nafasi yake ya kutawala huduma hizo inatishiwa na bodaboda.
Ili kutekeleza mageuzi haya kwa ufanisi, LATRA inahitaji Mtaalamu wa Usafiri wa Umma mwenye utaalamu wa kiufundi katika mipango ya usafiri mijini, usanifu na uundaji wa mifano ya usafiri wa umma, mageuzi ya kitaasisi na mifumo ya udhibiti, atakayeweza kuelekeza mabadiliko ya mitandao iliyopo ya usafiri kuwa mifumo ya usafiri wa umma iliyopangwa na endelevu.
2. Malengo ya Kazi
Lengo kuu ni kuisaidia LATRA kufanya mageuzi ya uendeshaji wa daladala katika Jiji la Dodoma kwa kutoa utaalamu wa kiufundi, mwongozo wa kimkakati, kuimarisha taasisi kupitia kujenga uwezo, na kutoa mapendekezo yanayoweza kutekelezwa.
Malengo mahususi ni pamoja na:
- Kusaidia LATRA kupitia, kuchambua, kusimamia na kukamilisha upembuzi yakinifu wa mageuzi ya daladala pamoja na tafiti nyingine zinazohusiana na masuala ya kiufundi.
- Kutoa ushauri wa kiufundi na mwongozo wa vitendo kuhusu mabadiliko ya waendeshaji binafsi kuwa vyombo vya kisheria vya pamoja, kwa mifumo mbalimbali ikiwemo vyama vya ushirika au kampuni.
- Kusaidia LATRA katika kubuni na kutekeleza hatua za mageuzi, zikiwemo mipango ya usafiri wa umma, uchambuzi na usanifu wa uendeshaji wa mfumo, uimarishaji wa taasisi na utawala, mipangilio ya utoaji leseni, mikataba ya huduma na mifumo ya ufuatiliaji.
- Kusaidia kujenga uwezo wa watumishi wa LATRA na wadau wakuu kuhusu mipango, uendeshaji, uchambuzi, udhibiti na utekelezaji wa mageuzi ya usafiri wa umma.
- Kuhakikisha mageuzi yanaendana na malengo mapana ya Mradi wa DIST, Mpango Kabambe wa Usafiri Jumuishi wa Dodoma na mamlaka ya udhibiti ya LATRA.
- Kupitia mipangilio ya sasa ya kitaasisi ya Serikali kwa ajili ya kutoa huduma endelevu za usafiri wa umma mijini katika Dodoma.
- Kuandaa mapendekezo na chati za muundo wa watumishi zinazounga mkono mfumo wa uendeshaji unaopendekezwa, pamoja na maelezo ya kawaida ya majukumu ya kazi kwa nafasi zilizobainishwa katika chati hiyo.
3. Wigo wa Kazi
Mshauri atatekeleza kazi zifuatazo, bila kujifungia katika orodha hii:
(i) Mapitio na Mchango wa Kiufundi
- Kupitia na kutoa mwongozo kuhusu Mpango Kabambe wa Usafiri Jumuishi ili kuwezesha utekelezaji wa hatua endelevu za usafiri wa umma ndani ya muktadha wa mpango huo katika Dodoma.
- Kupitia upembuzi yakinifu wa mageuzi ya daladala, machaguo ya mifumo ya biashara na athari zake za kiudhibiti.
- Kutathmini mikakati inayopendekezwa kama vile uanzishwaji wa vyama vya ushirika, utoaji wa leseni za kipekee za njia na matumizi ya teknolojia katika uendeshaji.
(ii) Msaada wa Sera na Udhibiti
- Kupendekeza mapitio muhimu ya sheria na kanuni ili kusaidia vyama vya ushirika na kampuni.
- Kutoa ushauri kuhusu uandaaji wa mifumo ya utoaji leseni na mikataba ya ukodishaji/konisheni kwa waendeshaji.
(iii) Mipango ya Mpito na Utekelezaji
- Kusaidia LATRA kuandaa mpango wa kina wa mpito kutoka kwa waendeshaji binafsi kwenda kwenye taasisi zilizopangwa.
- Kusaidia LATRA kubuni mipangilio ya kimkataba (kwa mfano, vipindi vya kufuatana kwa magari kwenye njia, mifumo ya malipo na viwango vya huduma).
- Kushauri kuhusu usanifu wa mifumo ya udhibiti wa nauli inayosawazisha uwezo wa abiria kumudu na uendelevu wa waendeshaji.
(iv) Kujenga Uwezo
- Kutoa mafunzo kwa watumishi wa LATRA kuhusu mipango, uendeshaji, usanifu na uchambuzi wa usafiri wa umma, usimamizi wa mageuzi, usimamizi wa uzingatiaji wa kanuni na mifumo ya ufuatiliaji.
- Kuendesha warsha kwa waendeshaji wa daladala na wadau ili kujenga uelewa na kupata uungwaji mkono.
(v) Ulinganifu na DIST na Mpango Kabambe
- Kuhakikisha mageuzi yanaendana na Mpango Kabambe wa Usafiri Jumuishi wa Dodoma na ujumuishaji wa baadaye wa BRT.
- Kutoa ushauri wa kiufundi kuhusu uratibu wa wadau na CCD, TARURA, TANROADS na taasisi nyingine.
(vi) Kuimarisha Mipangilio ya Kitaasisi kwa Ajili ya Kutoa Huduma za Usafiri wa Umma
- Kupitia taasisi za sasa za Serikali (katika ngazi zote) kwa kuzingatia ufanisi wa utoaji wa huduma za usafiri wa umma katika Dodoma.
- Kuandaa na kusimamia mchakato shirikishi na unaowezesha, utakaofikia mapendekezo ya mageuzi ya kitaasisi yanayoungwa mkono na chati za miundo ya taasisi na maelezo ya kawaida ya majukumu ya kazi, ili kuhakikisha utoaji wa usafiri jumuishi wa mijini katika Dodoma unakuwa na ufanisi na tija.
(vii) Masuala ya Jinsia na Ujumuishi
- Kujumuisha hatua za kuboresha usalama na upatikanaji wa huduma kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
- Kuhamasisha fursa za ushiriki wa wanawake katika ajira na usimamizi wa sekta ya usafiri wa umma.
4. Matokeo/Matoleo ya Kazi
Mshauri atawasilisha, angalau, matokeo yafuatayo:
- Ripoti ya Awali inayoeleza mbinu/mwelekeo wa utekelezaji, mpango wa kazi, utambuzi wa wadau na ratiba.
- Ripoti za Mapitio ya Uchunguzi na Tathmini ya Hali ya Msingi ya Usafiri wa Umma (Daladala).
- Ripoti ya mapitio yenye mapendekezo kuhusu upembuzi yakinifu wa daladala.
- Mapendekezo ya usanifu wa mfumo wa uendeshaji na biashara kwa ajili ya mpito kwenda kwenye vyama vya ushirika/kampuni.
- Mpango wa Mpito na Utekelezaji wa mageuzi ya daladala (ikiwemo utayari wa kuunganisha na BRT na mifumo mingine ya usafiri wa watu wengi).
- Mifumo ya Udhibiti, Mageuzi ya Kitaasisi na Mikataba — rasimu na matoleo ya mwisho.
- Mpango wa Kujenga Uwezo na Mafunzo (kwa watumishi wa LATRA na waendeshaji wa usafiri), ukiwemo moduli za mafunzo na ripoti za warsha.
- Ripoti ya mageuzi ya kitaasisi ya daladala inayopendekezwa pamoja na chati za miundo ya taasisi na maelezo ya kawaida ya majukumu ya kazi.
- Ripoti za Ushirikishwaji wa Wadau (mashauriano na waendeshaji, vyama vya madereva na mamlaka za jiji).
- Ripoti za kila mwezi na kila robo mwaka kuhusu shughuli zilizotekelezwa (zitawasilishwa ndani ya siku tano baada ya mwisho wa mwezi/robo mwaka).
- Kutoa ripoti za mara kwa mara za utafiti kuhusu uzoefu ulioshirikishwa/tafiti za mifano ya mbinu bora za mageuzi ya usafiri usio rasmi wa umma, urasimishaji wa usafiri wa paratransit na ujumuishaji wake katika mifumo yenye uwezo mkubwa katika miji inayoendelea.
- Ripoti ya mwisho ya kazi ikijumuisha mafunzo yaliyopatikana, changamoto na mapendekezo yanayoweza kutekelezwa.
Maelezo ya kila toleo la kazi yamefupishwa katika jedwali lifuatalo:
| Na. | Toleo la Kazi | Shughuli Kuu | Viashiria vya Utendaji | Njia za Uhakiki |
|---|---|---|---|---|
| 1 | Ripoti ya Awali | Kupitia nyaraka za mradi, kutambua wadau, mbinu za utekelezaji na mpango wa kazi. | Ripoti ya awali kuwasilishwa ndani ya muda uliokubaliwa; mbinu kuidhinishwa na mteja; mpango wa ushirikishwaji wa wadau kukamilika. | Ripoti ya awali iliyoidhinishwa |
| 2 | Ripoti za Uchunguzi wa Usafiri wa Umma na Mapitio ya Tathmini ya Hali ya Msingi | Kutathmini shughuli za sasa za daladala, hali ya magari, njia, mifumo ya fedha inayotegemea malengo ya kila siku, miundo ya umiliki, kumbukumbu za usalama na mapungufu ya sasa ya udhibiti. | Mapitio ya kina ya takwimu za hali ya msingi zinazohusu uendeshaji, njia na idadi ya magari; kubainisha mapungufu ya ufanisi wa soko na masuala ya usalama. | Ripoti ya tathmini ya hali ya msingi na kanzidata ya ramani za njia |
| 3 | Ripoti za Usanifu wa Mfumo wa Uendeshaji na Biashara | Kuandaa mifumo ya mpito kwenda kwenye taasisi za pamoja, ikiwemo kuhamia kwenye mishahara isiyobadilika, saa za kazi zilizopangwa, ukusanyaji wa nauli bila fedha taslimu na matumizi ya magari kwa pamoja. | Kupitia na kusasisha mifumo ya biashara inayopendekezwa kwa vyama vya ushirika/kampuni; tathmini ya uwezo wa kifedha wa mfumo mpya wa mishahara. | Ripoti za mapitio ya usanifu wa mfumo wa uendeshaji na biashara |
| 4 | Mifumo ya Rasimu na ya Mwisho ya Mageuzi ya Udhibiti na Taasisi | Kuandaa masasisho muhimu ya kanuni, mapendekezo ya sera, miongozo ya mikataba inayotegemea utendaji, mageuzi ya taasisi za Serikali na mahitaji mapya ya leseni kwa taasisi za pamoja. | Mapungufu ya udhibiti kubainishwa na masasisho kuandaliwa; vielelezo vya mikataba inayotegemea utendaji kuandaliwa; mfumo wa utoaji leseni kwa vyama vya ushirika kuidhinishwa; mageuzi ya taasisi pamoja na chati za miundo na maelezo ya kawaida ya majukumu ya kazi. | Hati ya mfumo wa udhibiti na taasisi pamoja na rasimu za mikataba ya waendeshaji |
| 5 | Ramani ya Urasimishaji na Mpito wa Daladala | Kuandaa mkakati wa utekelezaji wa awamu kwa ajili ya kurasimisha waendeshaji, kuboresha magari na kuweka msingi wa kiutendaji kwa ajili ya ujumuishaji wa baadaye na mifumo ya BRT. | Mpango wa mpito wa awamu kuandaliwa; mahitaji ya awali na ulinganifu wa kiutendaji wa ujumuishaji wa BRT na mifumo mingine ya usafiri wa watu wengi kubainishwa. | Mkakati wa Mpito na Ramani ya Utekelezaji |
| 6 | Mpango wa Kujenga Uwezo na Mafunzo | Kutathmini mapungufu ya ujuzi na kuandaa programu za mafunzo kwa watumishi wa LATRA (upangaji/usimamizi wa mfumo) na waendeshaji (utawala wa kampuni na usimamizi wa fedha). | Tathmini ya mahitaji ya mafunzo kukamilika; moduli kuandaliwa kwa LATRA na waendeshaji. | Mpango wa Kujenga Uwezo na vifaa vya mafunzo |
| 8 | Ripoti za Mashauriano na Wadau | Kufanya mashauriano na wamiliki wa daladala, vyama vya madereva, LATRA, halmashauri ya jiji, makundi ya wasafiri na watoa huduma za teknolojia wa sekta binafsi. | Idadi ya mikutano ya wadau iliyofanyika; maoni na uungwaji mkono wa waendeshaji kurekodiwa; ujumuishaji wa masuala ya jinsia na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi kuoneshwa. | Ripoti za mashauriano, orodha za mahudhurio na kumbukumbu za vikao |
| 9 | Mpango wa Mwisho wa Mageuzi, Ramani ya Utekelezaji na Uwasilishaji | Kuwasilisha ripoti za mwisho, miongozo ya udhibiti, mifumo ya mpito, miongozo ya kiutendaji na mawasilisho kwa menejimenti ya LATRA na wadau. | Ripoti ya mwisho kukubaliwa na mteja baada ya maoni yote kushughulikiwa; mifumo inayoweza kuhaririwa na miongozo ya kiutendaji kuwasilishwa. | Ripoti ya mwisho iliyoidhinishwa na wasilisho |
Ratiba ya matoleo ya kazi imeoneshwa katika jedwali lifuatalo (kwa kuzingatia makadirio ya kazi ya miezi 18):
| Na. | Toleo la Kazi | Muda |
|---|---|---|
| 1 | Ripoti ya Awali | Siku 14 baada ya kuanza kazi |
| 2 | Ripoti za Uchunguzi wa Usafiri wa Umma na Mapitio ya Tathmini ya Hali ya Msingi | Miezi 3 baada ya kuanza kazi |
| 3 | Ripoti za Mapitio ya Usanifu wa Mfumo wa Uendeshaji na Biashara | Miezi 6 baada ya kuanza kazi |
| 4 | Mifumo ya Rasimu na ya Mwisho ya Mageuzi ya Udhibiti na Taasisi | Miezi 9 baada ya kuanza kazi |
| 5 | Mpango wa Kujenga Uwezo na Mafunzo | Miezi 10 baada ya kuanza kazi |
| 6 | Ramani ya Urasimishaji na Mpito wa Daladala | Miezi 14 baada ya kuanza kazi |
| 7 | Ripoti za Mashauriano na Wadau | Katika kipindi chote cha kazi |
| 8 | Mpango wa Mwisho wa Mageuzi, Ramani ya Utekelezaji na Uwasilishaji | Kabla ya mwisho wa kazi (miezi 24)miezi baada ya kuanza kazi |
| 9 | Ripoti ya Maendeleo ya Kila Mwezi | Siku tano baada ya mwisho wa mwezi wa taarifa |
Mbinu ya Tathmini ya Utendaji
Mteja atafanya mapitio ya utendaji kila mwezi na kuandaa ripoti ya tathmini ya utendaji wa mwezi kufikia siku ya tano ya kila mwezi. Kuendelea kwa ushiriki wa mshauri na uchakataji wa malipo kutategemea mapitio na kukubaliwa kwa matoleo ya kazi yaliyokubaliwa.
5. Malipo, Muda na Mahali pa Kazi
- Malipo yatachakatwa kupitia LATRA na yatategemea kuwasilishwa kwa ripoti za kila mwezi na utendaji wa kuridhisha, kama utakavyothibitishwa na matoleo ya kazi au hatua muhimu zilizokubaliwa.
- Kazi inatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 24, ambacho kinaweza kuongezwa kulingana na utendaji na mahitaji ya mradi.
- Mshauri atakuwa Dodoma kwa miezi mitatu ya kwanza ya kazi na baadaye (miezi 21) atafanya kazi kwa asilimia 50 ya muda, pamoja na ziara za maeneo ya kazi kadiri zitakavyohitajika.
6. Utoaji wa Taarifa na Usimamizi
- Mshauri atawasilisha taarifa moja kwa moja kwa Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, LATRA, na katika shughuli za kila siku atafanya kazi kwa karibu na Mratibu wa LATRA wa Timu ya Utekelezaji wa Mradi wa DIST.
- Uratibu wa mara kwa mara utaendelezwa na Mratibu wa Mradi, Timu ya Benki ya Dunia na wadau husika wa Serikali.
7. Sifa na Uzoefu Unaohitajika
- Shahada ya uzamili katika Mipango ya Usafiri, Uchumi wa Usafiri na Usimamizi wa Usafirishaji wa Mizigo, Usafirishaji wa Mizigo na fani nyingine zinazohusiana.
- Uzoefu wa kitaaluma wa angalau miaka 5 katika mipango na mageuzi ya usafiri wa mijini/umma, na hasa kushiriki katika angalau miradi 2 ya mabadiliko ya sekta ya mabasi madogo au usafiri wa paratransit.
- Uzoefu uliothibitishwa katika usanifu na utekelezaji wa mifumo ya usafiri wa umma inayotegemea vyama vya ushirika/kampuni (ameshiriki katika miradi miwili inayofanana kama Mtaalamu wa Usafiri wa Umma ndani ya miaka 6 iliyopita).
- Uelewa wa mazingira ya usafiri wa mijini barani Afrika; uzoefu katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara utakuwa faida ya ziada.
- Uelewa mzuri wa mifumo ya udhibiti, sera za nauli na mageuzi ya kitaasisi.
- Uzoefu uliothibitishwa katika kujenga uwezo na kushirikisha wadau.
- Uwezo bora wa mawasiliano na uandishi wa ripoti kwa Kiingereza; ujuzi wa Kiswahili utakuwa faida ya ziada.
8. Vifaa na Msaada Utakaotolewa
- Nafasi ya ofisi, upatikanaji wa nyaraka husika za mradi na msaada wa uratibu na wadau.
- Usafiri wa kwenda maeneo ya kazi ili kuwezesha ushirikishwaji wa wadau.
- Watumishi wasaidizi wa kumtambulisha mshauri na kupanga uratibu wa mikutano na taasisi husika.
9. Usiri na Umiliki wa Matoleo ya Kazi
Takwimu, ripoti, uchambuzi, ramani, kanzidata na matokeo mengine yote yatakayozalishwa chini ya kazi hii yatabaki kuwa mali miliki ya kipekee ya LATRA na Serikali ya Tanzania. Mshauri hataruhusiwa kufichua, kuchapisha, kuzalisha upya au kushirikisha taarifa, matokeo ya uchambuzi au nyaraka zozote zinazohusiana na mradi kwa mtu au taasisi nyingine bila idhini ya maandishi ya awali kutoka LATRA. Wajibu huu wa usiri utaendelea kutumika katika kipindi chote cha kazi na kwa muda wa miaka mitatu (3) baada ya kukamilika kwake.
10. Mgongano wa Maslahi
Mshauri atatakiwa kutangaza mgongano wowote wa maslahi uliopo au unaoweza kujitokeza kabla au wakati wa utekelezaji wa kazi. Mshauri hatajihusisha na shughuli yoyote inayokinzana na majukumu yake chini ya mkataba huu, ikiwemo kutoa huduma kwa waendeshaji wa usafiri washindani au taasisi yoyote yenye maslahi ya moja kwa moja ya kifedha katika matokeo ya mageuzi, bila idhini ya maandishi ya awali kutoka LATRA. Kushindwa kutangaza mgongano wowote wa maslahi kutakuwa sababu ya kusitisha mkataba.
11. Viwango vya Maadili na Kanuni za Mwenendo
Mshauri atazingatia Mwongozo wa Kupambana na Rushwa wa Kundi la Benki ya Dunia na viwango vya maadili ya ununuzi wa umma vya Serikali ya Tanzania. Vitendo vyovyote vya udanganyifu, rushwa, njama za kupanga zabuni au vitendo vya kutumia shinikizo vitakuwa sababu za kusitishwa mara moja kwa mkataba na suala hilo kuwasilishwa kwa mamlaka husika.
Mshauri pia anatakiwa kuzingatia Viwango vya Mazingira na Jamii vya mradi, ikiwemo ahadi zinazohusiana na kuzuia Ukatili wa Kijinsia (GBV), Unyonyaji na Unyanyasaji wa Kingono (SEA), na Unyanyasaji wa Kijinsia (SH), kama ilivyoainishwa katika Mfumo wa Usimamizi wa Mazingira na Jamii (ESMF) wa Mradi wa DIST.

