Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA, DKT. SULUO: MADEREVA WA TEKSI MTANDAO TUMIENI FURSA YA AFCON 2027 KUTOA HUDUMA BORA
Imewekwa: 16 Sep, 2026
CPA, DKT. SULUO: MADEREVA WA TEKSI MTANDAO TUMIENI FURSA YA AFCON 2027 KUTOA HUDUMA BORA

CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amewataka madereva wa teksi mtandao nchini kutumia fursa zinazotarajiwa kujitokeza kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kujiandaa kutoa huduma bora, salama na za kuaminika kwa abiria na wageni watakaotembelea Tanzania.

CPA, Dkt. Suluo ameyasema hayo Septemba 15, 2026, kwenye Mkutano Mkuu wa kwanza wa Chama cha Madereva wa Teksi Mtandao Tanzania (TODA) uliofanyika Ukumbi wa mikutano wa Karimjee, Dar es Salaam.

CPA, Dkt. Suluo amesema, maandalizi ya AFCON 2027 yanapaswa kuanza mapema, kwa kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya wageni na abiria, hivyo kutoa fursa kwa madereva wa teksi mtandao kuongeza kipato kupitia huduma bora za usafirishaji.

“Kuelekea maandalizi ya AFCON 2027 kuna fursa nyingi kwa madereva wa teksi mtandao, kama wasafirishaji tunatakiwa kufahamu kuwa abiria na wageni wataongezeka, madereva wa teksi mtandao ndio watu wa kwanza kukutana na wageni watakaotembelea Tanzania, hivyo, mnapaswa kutumia fursa hii kuhakikisha wageni mnawapokea vizuri na kuwapatia huduma bora na kuacha taswira nzuri ya nchi kupitia huduma bora ya usafirishaji itakayotolewa,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Vilevile CPA, Dkt. Suluo amewataka madereva kuepuka kuwatoza abiria nauli kubwa na badala yake kutoa huduma zinazokidhi matarajio ya wateja, akisisitiza kuwa maandalizi ya kutoa huduma bora yanapaswa kuanza sasa.

“Kuelekea AFCON maandalizi tunaanza leo, mjitahidi kutoa huduma bora zitakazoacha tabasamu kwenye nyuso zao na kukidhi matarajio yao kwetu, kwani ninyi madereva ndiyo watu wa kwanza kukutana na wageni watakaotembelea nchi yetu kwenye AFCON 2027, hivyo mna wajibu wa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo ikiwemo kutomzidishia abiria nauli kwa tamaa ya kujiongezea kipato,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Katika hatua nyingine, CPA, Dkt. Suluo amewasihi madereva wa teksi mtandao kuzingatia Sheria na Kanuni za usalama barabarani, kuhakikisha vyombo vyao vina bima na leseni halali ya LATRA, pamoja na kuzingatia usalama wa abiria kuwa kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu yao.

 “Abiria anapokuwa ndani ya chombo cha usafiri, anakuwa amempa dereva dhamana ya usalama wake, hivyo ni muhimu kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo ikiwemo madereva Bodaboda kuvaa kofia ngumu na kuhakikisha usalama wa abiria hao unalindwa wakati wote wa safari ili kuepusha ajali za barabarani kwani kosa moja barabarani linaweza kugharimu uhai wa watu wengi,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Kwa upande wake, Bw. Ebony Ford, Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva wa Teksi Mtandao (TODA) ameiomba Serikali kuwawezesha kupata mafunzo yatakayowaongezea ujuzi wa kutumia teknolojia katika kazi zao, pamoja na mafunzo mengine yatakayowawezesha kutoa huduma bora za usafirishaji.

“Ili kufikia malengo yetu kuelekea maandalizi ya AFCON 2027, tunaiomba Serikali kuwawezesha madereva wa teksi mtandao kupata mafunzo yatakayowawezesha kuwaandaa kutoa huduma bora zaidi kuelekea michuano hiyo, pamoja na kuimarisha mchango wa madereva hao katika maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini”, amesema Bw. Ford.

Maandalizi ya AFCON 2027 yanatoa fursa muhimu kwa sekta ya usafiri wa teksi mtandao, hivyo ubora wa huduma, usalama wa abiria na utii wa Sheria na Kanuni ni mambo muhimu ambayo madereva wanapaswa kuyazingatia. Madereva wanapaswa kutumia fursa hiyo kutoa huduma za kitaalamu, zenye heshima na usalama, na kuhakikisha kila mgeni anayesafiri kwa teksi mtandao anaondoka akiwa na uzoefu mzuri na tabasamu usoni hivyo kujenga taswira nzuri ya Tanzania.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor