CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amewasihi wadau wa sekta ya usafiri ardhini kuchukua tahadhari wakati wa mvua kubwa za El Niño kwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzingatia maelekezo ya mamlaka kuhusu hali ya barabara na usalama wa safari.
Dkt. Suluo amesema hayo Septemba 24, 2026, kwenye mkutano na wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Akieleza athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Suluo amesema mvua kubwa zinaweza kusababisha mafuriko, maji kuvuka barabara, utelezi, mmomonyoko na maporomoko ya udongo au mawe, kuharibika kwa barabara, upepo mkali na ukungu unaopunguza uono wa madereva.
Amesema hali hiyo inahitaji maandalizi ya mapema kutoka kwa kila mdau, hivyo wanapaswa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na hali ya barabara kabla ya safari, ili waweze kuchukua hatua stahiki na kuepuka maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama.
Kwa upande wa wamiliki wa vyombo vya usafiri, Dkt. Suluo amewataka kuhakikisha magari yanafanyiwa ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara, hususan mifumo ya breki, matairi, taa, vioo na visafisha vioo (wipers), pamoja na kurekebisha hitilafu kabla ya safari.
Pia, amewataka madereva kuwa makini kwa kupunguza mwendo, kuongeza umbali kati ya vyombo na kuepuka maeneo yenye maji yanayotiririka kwa kasi au yenye kina kisichojulikana, “endapo hali ya barabara au mazingira ya safari si salama, safari isitishwe au iahirishwe. Usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara unapaswa kupewa kipaumbele,” amesisitiza.
Dkt. Suluo pia amewataka abiria kuwa sehemu ya ulinzi wa usalama wa safari kwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na barabara, kuepuka safari zisizo za lazima wakati wa mvua kubwa na kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa usalama, ikiwemo mwendokasi, uzidishaji wa abiria na uendeshaji usio salama. Aidha, amewasisitiza wamiliki na madereva wa magari yanayotoa huduma za usafiri wa wanafunzi kuweka usalama wa wanafunzi mbele na kuepuka maeneo yenye mafuriko, utelezi mkubwa au maji yanayotiririka kwa kasi
Katika hatua nyingine, Dkt. Suluo amewasihi wadau wote kushirikiana na Mamlaka ili kuhakikisha usafiri unaendelea kuwa salama wakati wote wa mvua za El Niño, huku wananchi wakihimizwa kutoa taarifa mapema wanapobaini hali inayoweza kuhatarisha usalama wa usafiri kwa kupiga simu LATRA saa 24 bila malipo kupitia 0800110019 au 0800110020, au kutuma ushahidi kupitia WhatsApp 0681300800

