Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA SULUO: SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMETUPAISHA KIUTENDAJI
Imewekwa: 19 Oct, 2023
CPA SULUO: SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMETUPAISHA KIUTENDAJI

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeiwezesha LATRA kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi na hivyo imeipa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

CPA Suluo amebainisha hayo kwenye Mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari uliofanyika Oktoba 19, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Golden Jubilee, jijini Dar es Salaam na ameeleza kuwa mafanikio ya LATRA yamejidhihirisha katika sekta tatu zinazodhibitiwa na Mamlaka hiyo ambayo ni sekta ya usafiri wa barabara, usafiri wa reli na usafiri wa waya.

Aidha, CPA Suluo amesema kuwa, katika usafiri wa barabara, kwa kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji iliongezeka kutoka leseni 230,253 hadi leseni 284,158 ikiwa ni sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.

“kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)( b) cha Sheria ya LATRA, Mamlaka inao wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na kufuta leseni za usafirishaji, hivyo Mamlaka hutoa leseni kila mwaka kwa vyombo vya usafiri kibiashara. Leseni hizi hutolewa baada ya mtoa huduma kukidhi masharti yanayotakiwa kwa aina ya huduma husika. Leseni hizi hutumika kutambua idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa,” ameeleza CPA Suluo.

Vilevile amesema kuwa, Mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vinavyodhibitiwa kwa lengo la kupata madereva wenye sifa na weledi kuendesha magari yanayotoa huduma kwa usafiri wa umma kwa kupima umahiri wao hasa maarifa waliyopata ili kuimarisha usalama, “Hadi, kufikia Septemba 30, 2023, madereva 17,990 wamesajiliwa na kuingiza taarifa zao kwenye kanzidata ya Mamlaka ambapo madereva 1,617 wamethibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa na LATRA. Miongoni mwa madereva hawa madereva wa mabasi wapatao 645 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho (identification button, i-button). Matumizi ya kitufe hicho ni kurahisisha utambuzi wa dereva anayeendesha gari kwa wakati husika kupitia mfumo wa VTS.”

Katika Usafiri wa Reli, CPA Suluo ameeleza kuwa Mamlaka, imeendelea kutoa mafunzo kazini kila mwaka kwa Wafanyakazi Muhimu wa Usalama katika uendeshaji wa reli (Safety Critical Workers) kwa TAZARA na TRC ili kuwaongezea ujuzi wa kutimiza majukumu yao kwa weledi na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 LATRA imepanga kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo unazingatiwa katika usafiri wa reli.

“Mafunzo ya aina hii husaidia kuwajengea uwezo wafanyakazi hao muhimu kuzuia ajali zitokanazo na makosa ya kibinadamu (Human Errors). Tathmini inaonesha kwamba, makosa ya kibinadamu katika uendeshaji wa shughuli za reli huchangia zaidi ya asilimia ya 85% ya ajali zote za treni kwa TRC na TAZARA. Hivyo, mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu,” amefafanua CPA Suluo.

Aidha, CPA Suluo ameeleza kuwa, LATRA imepiga hatua kubwa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo Mamlaka inatumia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kiudhibiti (RRIMS), Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo wa Tiketi Mtandao, Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App), Mfumo wa e-Mrejesho pamoja na Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Umma wa Kieletroni (NeST).

CPA Suluo amesema kuwa, Mfumo wa RRIMS unaopatikana kwa anwani ya https://rrims.latra.go.tz/login unamwezesha mteja kufanya maombi ya leseni ya usafirishaji kutokea mahali popote alipo na maombi yote yanayowasilishwa yanafanyiwa kazi siku hiyo na kuhakikisha anapata leseni chini ya saa 24. “RRIMS  imeunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali kama vile TRA, TIRA, NIDA, GePG na BRELA na pia imeunganishwa na mifumo ya wadau wengine kama vile watoa huduma wa tiketi mtandao ili kurahisisha utoaji huduma za Mamlaka kwa wananchi.”

Vilevile amesema LATRA imeanza kutumia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) tangu mwaka 2017 na hadi sasa, zaidi ya magari 9,420 yameunganishwa na mfumo huu ambapo, magari 7,620 yapo hai na yaendelea kutoa taarifa kupitia mfumo huu. “Mfumo umesaidia Kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinazotokana na mwendokasi, umepunguza madhara ya ajali zinazotokana na mwendokasi na umerahisisha uchunguzi wa ajali pale zinapotokea.”

Ameelezea mifumo mingine ni Mfumo wa Tiketi Mtandao ambao umesaidia kudhibiti upandishaji holela wa nauli. Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App) unaopatikana ‘Play Store’ kwenye simu zote za Android na unamwezesha mwananchi kupata taarifa za nauli za mabasi ya masafa marefu na mabasi ya mijini na Mamlaka inaendelea kuboresha huduma za mfumo huo ili kuwezesha abiria kutambua mwendo kasi wa gari.

CPA Suluo amesema Mamlaka pia imejiunga na inatumia Mfumo wa Serikali wa e-Mrejesho unapatikana kupitia https://emrejesho.gov.go.tz kwa ajili ya kupokea Malalamiko, Mapendekezo, Pongezi au Maulizo na hivyo amewasihi wananchi kutumia mfumo huo kuwasilisha maoni yao ambayo yatafanyiwa kazi ndani ya siku 21. Pia LATRA inatumia Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Umma wa Kieletroni (NeST) kwa ajili ya kutangaza na kuchakata zabuni mbalimbali na hivyo  amewashauri wazabuni wajisajili kwenye mfumo huo ambao unapatikana kwenye tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili kuweza kushiriki kwenye zabuni Serikalini.

CPA Suluo ameeleza kuwa, LATRA pia inajivunia kutekeleza dhana ya ushirikishaji wa wadau kwa vitendo ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, LATRA ilifanya jumla ya mikutano ya wadau 36 ikiwemo mikutano 9 ya kupokea maoni kuhusu mapitio ya nauli, mikutano 6 ya mabadiliko ya kanuni, mikutano 6 ya kutoa elimu kuhusu masuala kuidhibiti, mikutano 7 ya kutunza mazingira na kuimarisha usalama wa usafiri ardhini. Aidha, Mamlaka ilifanya mikutano 8 kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi kero mbalimbali kwenye usafiri wa barabara na reli.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo