Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAWAKALA WA LATRA WAASWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA UWELEDI
Imewekwa: 15 Sep, 2026
MAWAKALA WA LATRA WAASWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA UWELEDI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewaasa mawakala wanaotoa huduma ya leseni za usafirishaji kwa niaba ya Mamlaka kwa wasafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu (Bodaboda na Bajaji) kutekeleza majukumu yao kwa uweledi, uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.

Rai hiyo imetolewa na Bw. Denis Daudi, Afisa Leseni na Usajili LATRA, wakati wa semina elekezi kwa mawakala wa LATRA kutoka kampuni ya MA Enterprises, Septemba 7, 2026 Ofisi za LATRA, Dar es Salaam.

Bw. Daudi amesema, mawakala hao wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa viwango vinavyolingana na huduma zinazotolewa na LATRA, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa usahihi, uwazi na kwa wakati.

“Tunapowahudumia wateja wetu kule barabarani, tunategemea mawakala wetu wawahudumie wateja kama ambavyo Mamlaka inavyowahudumia. Wanapaswa kutoa huduma salama na yenye kuzingatia taratibu na misingi iliyowekwa,” amesema Bw. Daudi.

Amefafanua kuwa, miongoni mwa majukumu ya mawakala hao ni kusaidia kusajili taarifa za vyombo vya usafirishaji na wamiliki wake katika Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS), na baada ya taarifa hizo kuingizwa kwa usahihi katika mfumo, namba ya malipo (Control Number) hutengenezwa na kutumwa kwenye namba ya simu iliyosajiliwa ya mmiliki wa chombo.

“Wakala anatakiwa kuhakikisha taarifa za chombo zinasajiliwa kwa usahihi na kuhakikisha mmiliki anapata namba ya malipo na baada ya mmiliki kupata namba hiyo, jukumu la mmiliki ni kufanya malipo ya leseni ya chombo chake. Wakala hatakiwi kupokea fedha taslimu kutoka kwa dereva au mmiliki wa chombo,” amesema Bw. Daudi.

Aidha, Bw. Daudi amesisitiza kuwa LATRA haitarajii mawakala wake kujihusisha na vitendo vya rushwa au kupokea fedha taslimu kutoka kwa wateja, akieleza kuwa utoaji wa huduma unapaswa kuzingatia misingi ya uwazi, uadilifu na taratibu zilizowekwa na Mamlaka.

Kwa upande wake, Bw. Andrew Masenga, Wakala wa LATRA, amesema kuwa semina hiyo imewasaidia kuelewa kwa kina majukumu yao pamoja na namna bora ya kuyatekeleza katika maeneo yao ya kazi.

“Semina tuliyoipata itaenda kuboresha mfumo mzima wa utendaji kazi wetu kwa kuwa wafanyakazi wenzangu 28 wote wamepata semina elekezi, Pamoja na yote tumetambua na kukumbushwa maeneo muhimu ya majukumu yetu, hivyo tutaweza kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema Bw. Masenga.

LATRA imeendelea kutoa mafunzo, miongozo na maelekezo kwa mawakala wake kwa lengo la kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi kupitia mawakala zinafanyika kwa weledi, uadilifu na uwazi, huku zikizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Mamlaka.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor