Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAKABIDHI VIFAA MOI
Imewekwa: 12 Oct, 2026
LATRA YAKABIDHI VIFAA MOI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imekabidhi vifaa na mahitaji mbalimbali kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yaliyofanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026 na utekelezaji wa shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Augustus Fungo, Afisa Huduma kwa Wateja Mkuu LATRA Oktoba 9, 2026, amesema CSR hiyo inalenga kuwaunga mkono watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi, pamoja na wagonjwa wengine, wakiwemo waathirika wa ajali za barabarani, hususan waendesha pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda).

“Ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha jamii inanufaika na kile kidogo tulichonacho. Tunapaswa kutambua mahitaji ya wananchi na kushiriki katika juhudi za kuwasaidia, kwa sababu maendeleo ya taasisi yanapaswa kwenda sambamba na ustawi wa jamii inayotuzunguka,” amesema Bw. Fungo.

Aidha, Bw. Fungo amewahimiza waendesha bodaboda kuzingatia Sheria na Kanuni za usalama barabarani kwa hiari na kuchukua tahadhari ili kuepuka ajali zinazogharimu nguvukazi ya Taifa, zinazosababisha ulemavu na gharama kubwa za matibabu, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuwajibika katika kulinda maisha yake na ya watumiaji wengine wa barabara.

Kwa upande wake Dkt. Lemeri Mchome, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya LATRA kwa msaada huo ambao unachangia kuboresha huduma na kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili wagonjwa wanaopata matibabu katika taasisi hiyo.

“Tunashukuru sana LATRA kwa msaada mlioutoa kwa wagonjwa wetu ambao ni waathirika wa ajali za barabarani na watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi, gharama za matibabu si kila mtanzania anaweza kuzimudu hivyo Serikali inapoleta msaada kama huu inawasaidia kwa kiasi kikubwa.”amesema Dkt. Mchome.

Pia, Dkt. Mchome ameeleza kuwa kati ya asilimia 70 ya wagonjwa wanaopokelewa MOI kati yao asilimia 70 ni wahanga wa ajali za barabarani na kati ya hao asilimia 40 ni maafisa usafirishaji wanaotumia usafiri wa Bodaboda.

LATRA inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuimarisha ustawi wa jamii kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, pamoja na kuendeleza misingi ya uwajibikaji kwa jamii na utekelezaji wa Sera ya Uendelevu wa Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG).

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor