Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WATUMISHI LATRA WAASWA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU
Imewekwa: 13 May, 2026
WATUMISHI LATRA WAASWA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU

Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) wameaswa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kujenga utamaduni wa kukataa rushwa na kusimamia haki wanapotekeleza majukumu yao, hatua itakayochangia kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau wa sekta ya usafiri ardhini nchini.

Wito huo umetolewa na Bi. Marcella Salu, Afisa Mchunguzi Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakati wa mafunzo kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na kukuza uadilifu yaliyofanyika Aprili 25 na 26, 2026 katika ofisi za LATRA Tanzania Bara, yakiwahusisha watumishi wote wa Mamlaka.

Bi. Salu amesema ni muhimu kwa kila mtumishi kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma pamoja na miongozo mbalimbali ya kazi ili kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha uadilifu wa taasisi na kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Kila mtumishi anapaswa kuwajibika ipasavyo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na kufahamu athari za ukiukwaji wa taratibu hizo katika utendaji kazi wa taasisi. Ni muhimu watumishi kuwa na elimu kuhusu maadili na madhara ya rushwa mahala pa kazi ili kila mmoja anapotekeleza majukumu yake afahamu athari za kujihusisha na vitendo hivyo,” amesema Bi. Salu.

Aidha, watumishi wa LATRA walikumbushwa umuhimu wa kujenga utamaduni wa uwazi, haki na uwajibikaji mahala pa kazi ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mamlaka.

“Rushwa ni adui wa haki, hivyo kila mtumishi anapaswa kuchukia na kupinga vitendo vya rushwa, kwa kuwa huduma zinazotolewa na LATRA zinagusa wananchi wengi nchini, ni muhimu watumishi kuwa waadilifu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao,” amesisitiza Bi. Salu.

Naye Bi. Nancy Amani, Afisa Uhusiano LATRA, ameipongeza Menejimenti ya Mamlaka kwa kuandaa mafunzo hayo, yatakayowawezesha watumishi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuwakumbusha wajibu wao wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuepuka vitendo vya rushwa.

LATRA imeendelea kuweka mkazo katika kujenga mazingira ya kazi yanayozingatia uadilifu, uwazi na uweledi kwa watumishi wake kama sehemu ya kuimarisha utendaji kazi na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora, zenye haki na zinazoaminika.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor