Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA KUADHIMISHA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI NOVEMBA 2026
Imewekwa: 14 Nov, 2026
LATRA KUADHIMISHA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI NOVEMBA 2026

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi na wadau mbalimbali, inaandaa Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini yatakayofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 26 Novemba 2026 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, yakilenga kuimarisha usalama, ubora na uendelevu wa huduma za usafiri ardhini nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba 2026, CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amesema, maadhimisho hayo yanalenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya uchukuzi na wananchi kwa ujumla ili kujadili fursa, changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma za usafiri ardhini.

“Maadhimisho haya ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya usafiri ardhini, kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya pamoja itakayosaidia kuboresha huduma za usafiri, kuimarisha usalama na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Vilevile amesema, kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kuharakisha Usafiri Endelevu: Usafiri Salama, Rafiki kwa Mazingira na Jumuishi kwa Wote” (Accelerating Sustainable Transport: Safe, Green and Inclusive Mobility), inayosisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya usafiri inayozingatia usalama wa watumiaji, utunzaji wa mazingira na upatikanaji wa huduma kwa makundi yote ya jamii.

Aidha, amesema maadhimisho hayo yatafanyika sambamba na Siku ya Usafiri Endelevu Duniani, inayoadhimishwa tarehe 26 Novemba kila mwaka, na yanatarajiwa kuwakutanisha washiriki takribani 2,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Dkt. Suluo amesema, maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya bidhaa na huduma zinazohusiana na mnyororo wa thamani wa usafiri ardhini, yatakayo toa fursa kwa taasisi za umma na binafsi, kampuni za usafirishaji, watoa huduma za teknolojia na wadau wengine kuonesha ubunifu, teknolojia na suluhisho zinazochangia maendeleo ya sekta hiyo.

“Maadhimisho haya yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na kutoa fursa za kujenga mahusiano ya kibiashara na kubadilishana maarifa yatakayosaidia kuboresha huduma za usafiri ardhini. Juhudi hizi zinaendana na mwelekeo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 katika kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi,” amesema Dkt. Suluo.

Ameongeza kuwa makongamano na mijadala ya kitaalamu itakayofanyika wakati wa maadhimisho hayo itatoa nafasi kwa wadau kujadili namna ya kuongeza ufanisi wa huduma, kuimarisha mifumo ya usalama, kukuza matumizi ya teknolojia na kuendeleza mifumo ya usafiri inayozingatia utunzaji wa mazingira.

LATRA inawaalika wananchi na wadau wote wa sekta ya uchukuzi kushiriki katika maonesho na makongamano hayo kwa kujisajili na kupata maelezo zaidi kupitia barua pepe transportweek@latra.go.tz. Wadau pia wanahimizwa kutumia fursa hiyo kuwasilisha mawazo, uzoefu na ubunifu utakaosaidia kuboresha huduma za usafiri ardhini na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor