CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amesema jumla ya madereva 8,642 wamethibitishwa na Mamlaka huku wahudumu 4,664 wamesajiliwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 hadi 2025/26
CPA, Dkt. Suluo amebainisha hayo Septemba 24, 2026, wakati akiwasilisha mafanikio ya LATRA katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano na Waandishi na Wahariri wa Habari ulioandaliwa na Msajili wa Hazina na kufanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 hadi 2025/26 jumla ya madereva 15,547 walisajiliwa na kufanya mtihani kupitia Mfumo wa Kutahini Madereva (Drivers Testing System – DTS), ambapo madereva 8,642 tu ndio walifaulu mtihani huo na kuthibitishwa na LATRA sawa na ongezeko la asilimia 56,” amesema CPA, Dkt. Suluo.
Amefafanua kuwa, jumla ya madereva 15,547 walisajiliwa na kufanya mtihani kupitia Mfumo wa Kutahini Madereva (Drivers Testing System – DTS), ambapo madereva 8,642 tu ndio walifaulu mtihani huo na kuthibitishwa na LATRA sawa na ongezeko la asilimia 56.
Aidha, amesema uthibitishaji wa madereva hauishii kwenye mitihani pekee, bali LATRA hutumia pia mifumo ya TEHAMA, ikiwemo Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Madereva (VTS) na Kifaa cha Utambuzi wa Dereva (i-Button), kufuatilia mienendo ya madereva wanapokuwa barabarani. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha madereva wanaendelea kuzingatia Sheria na taratibu za usalama barabarani, hivyo kuchangia kuimarisha usalama wa huduma za usafiri na kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali.
Kwa upande wa wahudumu, Dkt. Suluo amesema LATRA imeandaa mtaala wa kozi fupi ya wiki moja yenye jumla ya saa 60, kwa kushirikiana na vyuo vya elimu, ili kuhakikisha wahudumu wanapata ujuzi unaohitajika katika kutekeleza majukumu yao. Mafunzo hayo yanatolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Biashara (CBE), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).
“Mafunzo haya yalianza kutekelezwa Januari 2024, ambapo jumla ya wanafunzi 656 walipata mafunzo na kufaulu. Hadi kufikia Juni 2026, jumla ya wanafunzi 7,216 walikuwa wamepata mafunzo na kufaulu. Aidha, idadi ya wahudumu waliowasilisha maombi na kusajiliwa na LATRA iliongezeka kutoka 137, sawa na asilimia 21, katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi 2,956, sawa na asilimia 77 na mwaka wa fedha 2025/26 wahudumu 4,664, sawa na asilimia 65, walikuwa wamesajiliwa na LATRA,” amesema CPA Dkt. Suluo.
Uthibitishaji wa madereva na usajili wa wahudumu ni takwa la kisheria linaloipa Mamlaka jukumu hilo kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(d) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413. Jukumu hili linalenga kuhakikisha huduma za usafiri wa abiria na mizigo zinatolewa na madereva na wahudumu wenye uweledi, uelewa wa Sheria, Kanuni na Taratibu za usafirishaji.

