Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE AWESO AIPONGEZA LATRA KWA UTENDAJI KAZI NA UBUNIFU WA MIFUMO
Imewekwa: 02 Jun, 2025
MHE AWESO AIPONGEZA LATRA KWA UTENDAJI KAZI NA UBUNIFU WA MIFUMO

Mhe. Jumaa Aweso (Mb), Waziri wa Maji ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa utendaji kazi na ubunifu wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo imerahisisha utoaji wa huduma kwa wadau.

Mhe. Aweso ametoa pongezi hizo Juni 02, 2025 alipotembelea banda la LATRA kwenye maonesho ya Wiki ya Mazingira yanayofanyika jijini Dodoma, viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete.

Akielezea mifumo hiyo, Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA alimueleza Mhe, Aweso kuwa, Mamlaka inatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kubuni na kutumia Mifumo ya TEHAMA inayoongeza tija ya utendaji kazi na usimamizi wa huduma.

Vilevile Bw. Pazzy amesema kuwa, ili kuongeza tija ya udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini pamoja na kuongeza wigo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi, LATRA imewezesha upatikanaji wa taarifa za mabasi kupitia Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaopatikana kwa anwani pis.latra.go.tz/ uliounganishwa na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) unaowasaidia abiria na wadau wa usafiri nchini kufahamu taarifa za mabasi yanayoelekea vituo vya mabasi vilivyo karibu yao na kuwawezesha wadau hao kufahamu mwendokasi na mahala lilipo basi husika.

Kwa sasa msafirishaji hana haja ya kufika ofisini kuchukua leseni yake bali anafuata taratibu zote kuanzia kuomba hadi kuchapa leseni yake yeye mwenyewe kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Reli na Barabara (RRIMS) unaopatikana kwa anwani ya rrims.latra.go.tz/ “, ameeleza Bw. Pazzy.

Aidha, Bw. Pazzy ameitaja mifumo mingine inayotumiwa na LATRA ni Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App), Mfumo wa Safari Tiketi  tiketi.latra.go.tz/ pamoja na Mfumo wa Kutahini Madereva (DTS).

LATRA inashiriki kwenye maonesho ya Wiki ya Mazingira jijini Dodoma kuanzia Juni 01 hadi 05, 2025 ambapo wadau wa sekta ya usafiri ardhini wanapatiwa elimu kuhusu kazi na majukukumu ya Mamlaka.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo