Bw. Abdallah Mitawi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za taksi mtandao nchini, ikiwemo kufanya ukaguzi wa mifumo hiyo na kuhakikisha taarifa zinazowasilishwa ni sahihi, kamili na zinapatikana kwa wakati.
Bw. Mitawi ametoa maelekezo hayo akimuwakilisha Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa Chama cha Madereva wa Taksi Mtandao Tanzania (TODA) uliofanyika Septemba 15, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Karimjee, Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kujadili maandalizi ya usafirishaji wa wageni kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na maendeleo ya huduma za taksi mtandao nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Prof. Mbarawa, Bw. Mitawi ameipongeza LATRA kwa kuendelea kuboresha huduma za usafiri wa taksi mtandao kwa kufanikisha utoaji wa leseni kwa mifumo 24 ya taksi mtandao, huku Serikali ikisisitiza kuwa ukuaji wa sekta hiyo unapaswa kwenda sambamba na usalama wa abiria, ubora wa huduma, ushindani wenye tija na matumizi sahihi ya teknolojia.
“LATRA mmefanya kazi kubwa kuhakikisha huduma hii inaendelea kuwa bora nchini lakini mnapaswa kuongeza ufuatiliaji wa huduma hizi na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza mnazipatia ufumbuzi wa haraka na kwa wakati huku mkifanya ukaguzi wa mifumo hiyo ili kuthibitisha usahihi wa taarifa zinazowasilishwa”, ameeleza Bw. Mitawi.
Vilevile ameisihi LATRA kuendelea kukutana na madereva, wamiliki wa mifumo ya taksi mtandao na wadau wengine ili changamoto za usafiri huo zitambuliwe na kutatuliwa bila kuathiri ubunifu, uwekezaji na ubora wa huduma.
Katika hatua nyingine, Bw. Mitawi amewaelekeza LATRA, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kukutana na viongozi wa TODA ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuona namna bora ya kuwawezesha ili waweze kufanya kazi zao pasipo bughudha.
Akizungumzia maandalizi ya AFCON 2027, Bw. Mitawi amesema taksi mtandao zitakuwa sehemu muhimu ya huduma za usafiri kwa wageni watakaofika nchini, hivyo wadau wanapaswa kujiandaa mapema, “Dereva wa taksi mtandao atakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukutana na baadhi ya wageni wetu pindi wanapofika viwanja vya ndege, kwa maana hiyo, dereva atakuwa pia balozi wa Tanzania na hivyo lazima tujiweke tayari na kuhakikisha tunatoa huduma bora na kujenga utamaduni wa uadilifu kwa wageni wetu.”
Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha ukuaji wa huduma za taksi mtandao kwa kuzingatia usalama, ubora wa huduma, ushindani, matumizi ya teknolojia, ajira na ustawi wa madereva. Kwa kutekeleza maelekezo hayo, LATRA inatarajiwa kuimarisha usimamizi wa huduma za usafiri wa taksi mtandao, kuhakikisha mifumo inawasilisha taarifa sahihi, kufanya ukaguzi unaohitajika na kutatua changamoto za wadau kwa wakati, hatua inayolenga kujenga huduma za taksi mtandao zilizo salama, za kisasa, zenye ushindani na zinazochangia ajira na maendeleo ya uchumi wa Taifa, wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa wageni kuelekea AFCON 2027

