Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS), unaojulikana kwa jina la Safari Tiketi, umeendelea kurahisisha huduma za usafiri ardhini kwa kuwawezesha abiria kujikatia tiketi za safari kwa urahisi, wakati wowote na mahali popote, bila kulazimika kufika katika ofisi za kampuni za mabasi. Hatua hiyo imechangia kuongeza ufanisi na kuboresha huduma za usafiri ardhini kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Septemba 24, 2026, katika mkutano wa Wahariri na Waandishi wa Habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Katika mkutano huo, Dkt. Suluo aliwasilisha mafanikio ya LATRA kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Suluo amesema, maboresho ya Mfumo wa Safari Tiketi yamewawezesha abiria kujikatia tiketi wakiwa mahali walipo, kuchagua muda wa kusafiri, kuchagua basi pamoja na daraja la huduma analohitaji, na kufanya malipo kwa njia ya mtandao au kupitia ofisi za mawakala au kampuni husika.
Vilevile amesema, hadi sasa watoa huduma 14 wa Tiketi Mtandao wameunganisha mifumo yao na Mfumo wa Safari Tiketi wa LATRA, hatua inayowawezesha abiria kukata tiketi zao za safari kwa njia ya kielektroni kwa wakati.
Dkt. Suluo amewataja watoa huduma hao kuwa ni Busbora Company Limited, Otapp Agency Company Limited, Abood Bus Service Limited, Duarani Innovate Limited, Shabiby Transporters, Hashtech Tanzania Limited, Iyishe Company Limited, Voltic Tanzania Limited, Web Corporation Tanzania Limited, Mkombozi Infotech Company Limited, Itule Company Limited, Sepa Tech Limited, Logix Company Limited na Global Light & Company Limited.
Aidha, amesema matumizi ya mifumo ya Tiketi Mtandao yameendelea kukua, hali inayochangia kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma, pia upatikanaji wa taarifa za tiketi na miamala kwa njia ya kielektroni unaosaidia ufuatiliaji wa shughuli za usafirishaji na kuimarisha udhibiti wa huduma za mabasi ya masafa marefu.
“Kipindi cha utekelezaji wa mfumo, idadi ya abiria na thamani ya miamala iliyorekodiwa kupitia mfumo huo imeongezeka kutoka abiria 7,112 wenye thamani ya Shilingi bilioni 226.29 mwaka 2022/23, hadi kufikia abiria 28,673 wenye thamani ya Shilingi bilioni 993.96 mwaka 2025/26,” amesema Dkt. Suluo.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa matumizi ya mifumo ya Tiketi Mtandao, jumla ya abiria milioni 62.18 walitumia mifumo hiyo. Kati yao, abiria milioni 59.27, sawa na asilimia 95.3, walilipa nauli kwa fedha taslimu, huku abiria milioni 2.91, sawa na asilimia 4.7, wakitumia njia za malipo ya mtandao.
LATRA inaendelea kutekeleza jitihada za Serikali za kuimarisha matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidigiti katika usafiri ardhini ili kuhakikisha abiria wanapata huduma salama, rahisi, za uhakika na zenye ufanisi. Mifumo hiyo inaendelea pia kutumika kuimarisha uwazi, uwajibikaji, ufuatiliaji na udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini nchini.

