Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

TODA YAIOMBA SERIKALI KUWAJENGEA UWEZO MADEREVA WA TAKSI MTANDAO KUELEKEA AFCON 2027
Imewekwa: 15 Sep, 2026
TODA YAIOMBA SERIKALI KUWAJENGEA UWEZO MADEREVA WA TAKSI MTANDAO KUELEKEA AFCON 2027

Chama cha Madereva wa Taksi Mtandao Tanzania (TODA) kimeiomba Serikali kuendelea kuwawezesha madereva wa taksi mtandao kwa kuwajengea uwezo na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya usafiri kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa TODA uliofanyika Septemba 15, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Karimjee, Dar es Salaam, Bw. Ebony Ford, Katibu Mkuu wa TODA, amesema maandalizi ya AFCON yanahitaji madereva na wamiliki wa mifumo ya taksi mtandao kujiandaa mapema ili kutumia fursa zitakazotokana na kuongezeka kwa wageni na mahitaji ya huduma za usafiri nchini.

Ameongeza kuwa, moja ya maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele ni matumizi ya mifumo ya taksi mtandao, hususan katika suala la lugha, ili kuwawezesha madereva kuwahudumia wageni watakaotoka katika nchi mbalimbali duniani. Amesema mifumo hiyo inapaswa kuboreshwa ili iwe rafiki kwa watumiaji na iweze kukidhi mahitaji ya wateja kutoka mataifa na mazingira tofauti.

“AFCON itahusisha watu wa mataifa mbalimbali hivyo tunaomba Serikali itupatie mafunzo kwa vitendo ili na sisi tuweze kutumia teknolojia yenye lugha mbalimbali kuwahudumia wadau wa michezo watakaoshiriki na hii itatusaidia kutanua wigo wa fursa kipindi chote cha michuano hiyo,” amesema Bw. Ford.

Aidha, ameiomba Serikali kushirikiana na TODA katika kuandaa warsha na makongamano ya kuwajengea uwezo madereva, hasa kuhusu namna bora ya kuwahudumia wateja kwa ukarimu, uweledi na viwango vinavyokubalika kimataifa. Kwa mujibu wa Bw. Ford, maandalizi hayo ni muhimu kwa kuwa dereva wa taksi mtandao atakuwa sehemu ya uzoefu wa mgeni kuhusu huduma na ukarimu wa Tanzania.

Katika hatua nyingine, Bw. Ford ameomba kuwezeshwa kwa mifumo rafiki itakayorahisisha madereva wa taksi mtandao kupata bima ya afya pamoja na huduma za hifadhi ya jamii, ili kuhakikisha kuwa kazi yao haiwajengei kipato cha leo pekee bali pia inawaandalia madereva usalama na ustawi wa baadaye. Aidha, ameomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza kamisheni ya kodi kutoka asilimia 25 hadi asilimia 20, ikijumuisha kodi na mapato ya mfumo, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza tija kwa madereva.

Akizungumzia maandalizi kuelekea AFCON 2027, Bw. Ford amesema madereva wa taksi mtandao wana jukumu la kuhakikisha wanatumia ipasavyo fursa zitakazotokana na ujio wa wageni, jambo linalohitaji maboresho katika mifumo na huduma ili kuweza kuwahudumia wateja kwa viwango vya hali ya juu huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa utoaji wa huduma za usafiri kupitia mifumo ya taksi mtandao.

Mkutano huo wa TODA umefanyika katika kipindi ambacho huduma za taksi mtandao zimeendelea kuwa sehemu muhimu ya sekta ya usafiri nchini ikiwezesha watumiaji wa huduma hiyo kufika maeneo mbalimbali kwa urahisi ikiwemo hospitali, shuleni, maofisini na kadhalika.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor