Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imepiga hatua katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za leseni za usafirishaji, ambapo idadi ya leseni zinazotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo na magari ya kukodi imeongezeka kwa asilimia 146.1, kutoka leseni 239,953 mwaka wa fedha 2021/22 hadi 590,468 mwaka wa fedha 2025/26.
Hayo yameelezwa na CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, Septemba 24, 2026, alipozungumzia mafanikio ya LATRA katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Akifafanua ongezeko hilo, Dkt. Suluo amesema ukuaji wa leseni hizo una wastani wa asilimia 27.2 kwa mwaka, hali ambayo imeenda sambamba na hatua mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa huduma za leseni na kurahisisha mazingira ya utoaji wa huduma za usafirishaji nchini.
“Ongezeko la leseni za magari ya abiria na mizigo ni sawa na asilimia 146.1, wastani wa ukuaji wa asilimia 27.2 kwa mwaka, unaoonesha hatua zilizopigwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za leseni na kurahisisha mazingira ya utoaji wa huduma za usafirishaji nchini,” amesema Dkt. Suluo
Aidha, amesema Serikali ilifanya marekebisho mwaka 2023 ya Kanuni za LATRA za Huduma za Magari ya Kukodi za mwaka 2020 (GN Na. 78 ya tarehe 7 Februari 2020), kwa kuruhusu mawakala walioidhinishwa kutoa huduma za leseni za LATRA kwa vyombo vya usafiri wa kukodi. Marekebisho hayo yaliwezesha makundi manne ya mawakala ambayo ni kampuni, vyama vya ushirika, taasisi za umma na watu binafsi kushiriki katika utoaji wa huduma hizo.
Amefafanua kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu cha utekelezaji wa marekebisho hayo, kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 hadi 2025/26, LATRA imetoa vyeti kwa mawakala 100, wakiwemo kampuni 69, vyama vya ushirika saba, taasisi za umma 23, zikiwemo Serikali za Mitaa na Shirika la Posta Tanzania, pamoja na mtu mmoja binafsi.
Vilevile amesema jukumu la mawakala hao ni kusaidia kusajili taarifa za vyombo vya usafirishaji na wamiliki wake katika Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) ambapo baada ya taarifa kuingizwa kwa usahihi katika mfumo, namba ya malipo hutengenezwa na kutumwa kwenye namba ya simu iliyosajiliwa ya mmiliki wa chombo.
Ameongeza kuwa uwepo wa mawakala hao umechangia kurahisisha zaidi upatikanaji wa huduma za leseni, ambapo wameweza kutoa leseni za pikipiki za magurudumu mawili na matatu (bodaboda na bajaji) kwa wastani wa asilimia 70 na kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 7.9, kati yake Shilingi bilioni 2.0 zilirudishwa kwa mawakala hao kama kamisheni.
Kwa ujumla, ongezeko hilo la leseni linaakisi ukuaji wa shughuli za usafiri ardhini na jitihada zinazoendelea za LATRA kuboresha mifumo ya utoaji huduma. Mamlaka inaendelea kuhakikisha vyombo vinavyotoa huduma za usafirishaji vinakuwa na leseni halali na kuzingatia Sheria, Kanuni na masharti yaliyowekwa, huku ikiboresha zaidi mifumo na njia za utoaji huduma ili kufanya mchakato wa kupata leseni kuwa rahisi, wa haraka na unaowafikia wadau kwa ufanisi

