Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WASAFIRISHAJI KUWANIA TUZO ZA WATOA HUDUMA BORA ZA USAFIRI ARDHINI 2026
Imewekwa: 14 Nov, 2026
WASAFIRISHAJI KUWANIA TUZO ZA WATOA HUDUMA BORA ZA USAFIRI ARDHINI 2026

Watoa huduma za usafiri ardhini wanatarajiwa kuwania Tuzo za Watoa Huduma Bora na Salama za Usafiri Ardhini 2026, zitakazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kutambua na kupongeza watoa huduma waliofanya vizuri katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026. Tuzo hizo zitatolewa wakati wa Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini, yatakayofanyika kuanzia Novemba 24 hadi 26, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Amesema hayo CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA kwenye mkutano na waandishi wa habari Oktoba 23, 2026, jijini Dar es Salaam, ambapo amesema tuzo hizo ni sehemu ya jitihada za Mamlaka za kuhamasisha ushindani wenye tija na ufanisi miongoni mwa watoa huduma, kuimarisha uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia sekta ya usafiri ardhini, pamoja na kuboresha ubora na ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

“LATRA inaendelea kuratibu tuzo za watoa huduma bora za usafiri ardhini kwa lengo la kuimarisha ushindani wenye tija na ufanisi, kutambua na kuwapongeza watoa huduma wanaofanya vizuri, pamoja na kutoa fursa kwa watumiaji wa huduma za usafiri kushiriki katika kutathmini ubora wa huduma wanazopatiwa. Tuzo hizi zinalenga kuhamasisha madereva na wahudumu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kuchochea ubunifu katika utoaji wa huduma za usafiri ardhini na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs 2030),” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Dkt. Suluo ameeleza kuwa, tuzo hizo zitahusisha makundi 10 yanayowakilisha huduma mbalimbali zinazodhibitiwa na LATRA. Makundi hayo ni wasafirishaji wa mabasi ya masafa marefu, madereva wa mabasi ya masafa marefu, wahudumu wa mabasi ya masafa marefu, watoa huduma za teksi mtandao, watoa huduma za mifumo ya tiketi mtandao, watoa huduma za magari maalumu ya kukodi (Special Hire), watoa huduma za mifumo na vifaa vya kufuatilia mwenendo wa magari (VTS/VTD), watoa huduma za usafiri wa reli na wawezeshaji wa huduma zinazosimamiwa na LATRA.

Aidha, amesema washiriki katika kila kundi watatathminiwa kwa kutumia vigezo tisa vya jumla vinavyolenga kupima ubora wa huduma, usimamizi na ufanisi wa uendeshaji, huku kila kundi likiwa na vigezo mahususi vinavyozingatia aina ya huduma inayotolewa.

“Vigezo vya jumla vitakavyozingatiwa ni usimamizi bora wa vyombo vya usafiri, usimamizi wa huduma za usafiri ardhini, usimamizi wa wafanyakazi, uhakika wa huduma, usalama na ubora wa huduma kwa wateja, ubunifu na matumizi ya teknolojia, mwendelezo wa huduma katika kipindi cha tathmini, uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu pamoja na utunzaji wa mazingira. Kila kundi litakuwa na vigezo mahususi ili kuhakikisha tathmini inazingatia majukumu na viwango vinavyohusika na aina ya huduma inayotolewa,” amefafanua CPA Dkt. Suluo.

Ameongeza kuwa, wananchi na wadau wa sekta ya usafiri ardhini watapata fursa ya kushiriki katika kuwapigia kura watoa huduma watakaofikia hatua ya mwisho ya mchakato wa tathmini, na upigaji kura umepangwa kufanyika kwa siku 14, kuanzia tarehe 1 hadi 14 Novemba 2026, kupitia dodoso litakalowekwa kwenye tovuti rasmi ya LATRA, www.latra.go.tz, pamoja na tovuti ya maadhimisho transportweek@latra.go.tz na mitandao ya kijamii ya Mamlaka.

Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Sura ya 413, kimeipa Mamlaka jukumu la kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma wanaodhibitiwa. Utekelezaji wa jukumu hilo unalenga kuhakikisha ushindani unachochea ubora, ubunifu na ufanisi katika sekta ya usafiri ardhini, huku ukinufaisha watumiaji wa huduma hizo.

Kupitia tuzo hizo, LATRA inalenga kuendeleza utamaduni wa ubora na uwajibikaji miongoni mwa watoa huduma, kuhamasisha uzingatiaji wa sheria na matumizi ya teknolojia, pamoja na kuweka kipaumbele katika usalama wa abiria na mizigo, uhifadhi wa mazingira na utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor