Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MHE. BALOZI DKT. BATILDA BURIANI, MKUU WA MKOA TABORA KATIKA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA USALAMA WA RELI TAREHE 09 OKTOBA, 2023, CHUO CHA RELI, TABORA.
10 Oct, 2023 Pakua

Bi. Stella J. Katondo, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira, Wizara ya Uchukuzi, Unayemuwakilisha Katibu Mkuu Uchukuzi,

Prof. Ahmed Mohammed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi - LATRA,

CPA Habibu Juma Suluo, Mkurugenzi Mkuu -LATRA,

Ndugu Damas A. Mwajanga, Mkuu wa Chuo cha Reli – Tabora, Unayemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu TRC,

Wawakilishi wa Wakandarasi na Washauri Waelekezi,

Wadau wote wa usafiri wa reli mlioko hapa,

Ndugu Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uhai, afya njema na fursa ya kukutana hapa kwenye viwanja hivi vya stesheni ya reli Tabora kwa lengo la kufungua rasmi Wiki ya Usalama wa Reli kwa Mwaka 2023 yenye kaulimbiu “USALAMA UNAAZA NA WEWE; CHUKUA TAHADHARI” (“SAFETY BEGINS WITH YOUR ATTITUDE; ALWAYS BE CAREFUL”).

 Maadhimisho haya yanafanyika katika Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Mashirika ya Reli ya Kusini mwa Afrika (Southern African Railways Association, yaani SARA) ambapo kwa upande wa Tanzania, maadhimisho haya yanafanyika kitaifa hapa Mkoani Tabora.

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Pamoja na Tanzania kuwa Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Mashirika ya Reli ya Kusini mwa Afrika (SARA). SARA ni moja kati Jumuiya tanzu za SADC zilizoanzishwa ili kuratibu maendeleo ya miundombinu katika sekta ya usafiri kwa njia ya Reli.  SARA iliundwa mwaka 1996 kwa kuzingatia itifaki ya 13.13 ya SADC ili kuratibu maendeleo ya usafiri wa reli. Secretariet ya SARA ipo jijini Harare katika nchi ya Zimbabwe. Na shughuli zake zinasimamiwa na Bodi ya SARA na Tanzania ina wajumbe watatu ambao ni Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA na Mkurugenzi Mkuu wa TRC.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Nimefahamishwa kuwa kaulimbiu ya wiki ya usalama wa Reli kwa mwaka huu wa 2023, itatekelezwa kupitia kampeni ya kuongeza uelewa na tahadhari za usalama wa reli kwa wananchi katika Nchi zote wanachama wa SARA ili kuelewa mazingira hatarishi na hivyo kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika. Vilevile, nimefahamishwa kuwa kaulimbiu hii itadumu kwa mwaka mzima hadi wiki ya usalama wa reli mwaka, 2024. Aidha, shughuli za kuelimisha umma zitakuwa endelevu.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua vyema umuhimu wa ulinzi na usalama wa miuondombinu ya reli.  Serikali imeendelea kujenga miundombinu mipya ya reli na kuboresha iliyopo ili uendeshaji wa shughuli za reli uwe na tija. Usalama wa reli ndiyo kichocheo kikubwa cha uchumi wetu hapa Nchini, na eneo zima la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika kwa jumla.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Ili kuhakikisha usafiri wa reli unakua salama na wenye tija,  Serikali ilitunga Sheria ya Reli Na. 10 ya Mwaka 2017. Sheria hii imejikita katika usalama na ulinzi wa miundombinu ya reli, pia imeweka bayana kuchukuliwa hatua kwa yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya kuhujumu miundombinu ya reli na kuhatarisha usalama wa reli zetu. Aidha, Sheria ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ya Mwaka 1995 imeainisha jukumu la Serikali kwenye kuchukua hatua za udhibiti dhidi ya uharibifu na uhujumu wa miundombinu na huduma za reli.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Katika kuongeza ufanisi na tija kwenye sekta ya usafiri wa reli, Serikali pia imefanya marekebisho ya Sheria ya Reli Na. 10 ya Mwaka 2017 kwa kuruhusu ubia na uwekezaji wa sekta binafsi kwenye utoaji wa huduma za reli. Kwa sasa, mchakato wa kuaandaa Kanuni ili sekta binafsi kutumia reli Nchini, yaani Open Access Regulations, unaendelea. Rasimu ya kwanza imeshaandaliwa na hivi karibuni itawasilishwa kwa wadau kupata maoni yao ya kuiboresha kabla haijaanza kutekelezwa. Hili litafanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala bora wa kushirikisha wadau kabla ya Serikali kufanya maamuzi yatakayowagusa. Hata hivyo, katika kujenga mazingira bora ya kuvutia uwekezaji wa watoa huduma mbalimbali, suala la usalama wa reli litaendelea kuwa la msingi na kupewa kipau mbele.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Pamoja na Sheria hizo, Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana ya uchukuzi, imeandaa na inatekeleza Kanuni zaidi ya 12 kwa ajili ya kuhakikisha utaratibu wa uendeshaji wa shughuli za reli unakuwa salama na unazingatia kikamilifu maslahi mapana ya kiuchumi.

Pamoja na jitihada hizi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambaye ndiye Mdhibiti wa sekta ya usafiri wa reli hapa Nchini ikiwa na lengo la kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu za usalama  katika sekta ndogo ya reli vinazingatiwa.

LATRA imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa weledi na imehakikisha matakwa ya usalama na kiuchumi katika reli yanazingatiwa kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara. Vilevile, Mamlaka hii imekuwa ikihakikisha kunakuwa na huduma bora za usafiri wa reli zinazoweza kufikiwa na watumiaji wa hali zote, hususan wenye vipato vya chini.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza LATRA kwa hatua wanazochukua na kulielekeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuboresha Mfumo wa Tiketi Mtandao kwa abiria wa treni ili wajikatie tiketi zao wenyewe popote walipo kwa njia ya mtandao. Haya pia ni maagizo ya Serikali yaliyosisitizwa na Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, alipokuwa akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya TRC hivi karibuni. Mambo haya yamewezekana kwenye usafiri wa mabasi zaidi ya 8,500 Nchini, hatuoni sababu ya kutowezekana kwa TRC. Kwa ujumla, tunaona mabadiliko makubwa katika sekta ya reli yanakuja hapa Nchini. Kwa hili nawapongeza sana LATRA. Endeleeni kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, na kila mmoja atimize wajibu wake ili Watanzania wafurahie huduma bora na salama wa usafiri wa reli.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Uwepo wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Sheria mbalimbali umesaidia sana kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali na maafa yatokanayo na matumizi mabaya ya vyombo vya usafirishaji. Ajali zinapungua, si kuisha kabisa, kwa sababu kuna majanga mengine yapo nje ya uwezo wetu; mfano mafuriko, tetemeko la ardhi na kadhalika.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Tunapoadhimisha wiki hii ya usalama wa reli, nawasihi Wananchi wote na madereva wa vyombo vya moto kuchukua hadhari wanapopita kwenye makutano ya reli na barabara. Vilevile, tuwe walinzi wa miundombinu ya reli kwa maendeleo ya Nchi yetu. Aidha, katika maeneo yote ambayo alama za usalama wa reli zimeondolewa, tunasisitiza ziwekwe upya mapema kwa ajili ya kuimarisha usalama wa treni, abiria na mali zao.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Napenda  kutumia fursa hii kuwajulisha wadau wetu wote wa usafiri wa reli kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita, chini  ya Uongozi mahiri wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kuhakikisha usafiri wa reli unaendelea kuwa salama na wa kutumainiwa katika kuleta maendeleo ya Nchi yetu, Jumuiya ya nchi za SADC na Afrika kwa jumla.

Usalama wa reli ni suala mtambuka linahitaji ushirikiano wa pamoja kutoka Idara za Serikali, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Wadau wa Sekta na Wanachi kwa ujumla. Hivyo, ninawasihi tushirikiane ili kuhakikisha usafiri wa reli unaendelea kuwa bora, salama na wenye gharama nafuu katika kusafirisha mzigo mkubwa kwa wakati mmoja.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Nilipofika kwenye viwanja hivi, niliambiwa kuwa kuna maonesho yanaendelea hapa nami nikapata fursa ya kupita kwenye mabanda ya maonesho hayo. Kwa hakika, nimejionea na kujifunza, kutoka kwa taasisi zilizoshiriki maonesho haya, masuala ambayo yameniongezea uelewa wa mfumo wa usafiri wa reli. Nimeambiwa, taasisi hizi ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambaye ndiye Mdhibiti wa Sekta ya Reli Nchini, Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na wadau wengine kutoka sekta za umma na binafsi watakuwepo hapa wiki nzima wakitoa elimu kwa Umma kuhusu usalama wa usafiri wa reli pamoja na mambo mengine ambayo yatawasaidia wananchi pindi wanapotumia usafiri huu au wanapopita kwenye miundombinu ya reli.

Nami nitumie fursa hii kuwakaribisha wananchi wote wa hapa Tabora na Wilaya zake, pia mikoa ya jirani kufika kwenye viwanja hivi vya Stesheni kujifunza bila malipo kutoka kwa wadau wa usafiri wa reli. Mwambie rafiki, ndugu, jamaa na jirani yako afike hapa maana elimu watakayoipata itawasidia katika mazingira yao.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli, 2023 yamefunguliwa rasmi.

 

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo