Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MHE. DKT. ALLY POSSI, NAIBU KATIBU MKUU UCHUKUZI KATIKA UFUNGAJI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA USALAMA WA RELI TAREHE 13 OKTOBA
14 Oct, 2023 Pakua

Bi. Aisha Churu, Katibu Tawala Wilaya Tabora,

Bi. Stella J. Katondo, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira ya Uchukuzi, Wizara ya Uchukuzi,

Ramadhani Kateti, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Tabora,

Syllivester Yaredi, Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora,

Menejimenti ya Wizara ya Uchukuzi,

Bi. Vumilia Nyamoga, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknologia,

Bw. Abdul Dachi, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha,

Prof. Ahmed Mohammed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi - LATRA,

Mha. Hanya Mbawala, Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu - LATRA,

Bw. Damas A. Mwajanga Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Reli Tanzania, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu - TRC,

Bw. Sadiki Anthony Meneja Usalama wa Reli, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji - TAZARA,

BW. Waziri O. Waziri, Meneja TMA Kanda ya Magharibi  Bw.

Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tabora,

Wajumbe wa Bodi ya Chuo cha Reli (TIRTEC),

Wawakilishi wa Wakandarasi na Washauri Waelekezi wa Miradi ya Miundombinu ya Reli,

Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Usalama wa Reli,

Wadau wote wa usafiri wa reli mlioko hapa,

Ndugu Wanahabari,

Mabibi na Mabwana.

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA…….

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima, afya njema na kutupatia fursa ya kukutana hapa kwenye viwanja hivi vya Taasisi ya Teknolojia ya Reli Tanzania (TIRTEC) Tabora kwa lengo la kuadhimisha kilele cha Wiki ya Usalama wa Reli 2023 ambayo hufanyika mwezi Oktoba, kila mwaka. Maadhimisho haya yamefanyika kitaifa hapa Tabora na yameadhimishwa pia katika Nchi zote wanachama wa Shirikisho la Reli za Kusini mwa Afrika (SARA) ambao pia ni wanachama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Pili, na kipekee kabisa namshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na mageuzi makubwa anayoyaongoza katika kukuza uchumi wa Nchi yetu huku akizingatia mchango wa sekta binafsi na wadau wote wa maendeleo. Mfano dhahiri wa hivi karibuni ni mageuzi aliyoyafanya katika Sekta ya Uchukuzi ambapo ameamua kuivunja Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kuunda Wizara mbili; yaani Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi ili kurahisisha usimamizi wa sekta, kuharakisha maamuzi, kuongeza ufanisi na kuwaletea wananchi maendeleo kwa haraka.

Katika mageuzi haya, mimi  binafsi na kwa niaba ya familia yangu, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe. Rais kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi kuanzia tarehe 30 Agosti, 2023. Ninamuahidi kwa dhati Mhe. Rais kwamba nitajitahidi kwa uwezo wangu wote kutekeleza majukumu yangu kwa weledi, umahiri na umakini wa hali ya juu ili kuhakikisha sekta ya uchukuzi inakuwa na kuleta tija katika uchumi wetu. Naomba nitumie fursa hii pia kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa Wizara ya Uchukuzi, kumpongeza sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha sekta hii ya usafiri wa reli hapa nchini na kuhakikisha inahudumia watanzania wengi kwa gharama nafuu.

Aidha, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitoishukuru Kamati ya Maandalizi ya shughuli hii. Kwa hakika Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho haya imenipa heshima kubwa ya kuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha madhimisho ya wiki ya usalama wa reli kwa mwaka huu wa 2023. Asanteni sana.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli mwaka huu katika Nchi zote wanachama wa SARA ni “USALAMA UNAANZA NA WEWE; CHUKUA TAHADHARI” (“SAFETY BEGINS WITH YOUR ATTITUDE; ALWAYS BE CAREFUL”). Kaulimbiu hii inabeba ujumbe muhimu sana katika suala zima la usalama wa usafiri huu.

Nimeambiwa kuwa, wiki hii imeadhimishwa kwa kutumia kaulimbiu hii katika kampeni za uelimishaji umma kuhusu tahadhari za kiusalama ambazo zimefanyika kwenye shule mbalimbali hapa Nchini, kwenye vituo vya treni, ndani ya treni za abiria na maeneo ya ushoroba wa Reli. Aidha, nimeambiwa zoezi hili sio la wiki hii pekee, bali ni zoezi endelevu. Nazipongeza sana taasisi zote zilizoshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya na hasa zile zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi, na kuwa na mabanda ya kutoa elimu katika viwanja hivi chini ya Uongozi wa Wizara yetu. Hawa ni pamoja na LATRA, NIT, TAZARA, TRC na TMA. Hongera sana!

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Ukiitafakari kaulimbiu hii, “USALAMA UNAANZA NA WEWE; CHUKUA TAHADHARI” (“SAFETY BEGINS WITH YOUR ATTITUDE; ALWAYS BE CAREFUL”) utaona inabeba ujumbe mkubwa sana, na hasa ikielekeza katika maisha yetu ya kila siku.

Kila kitu tunachokifanya tunapaswa kwanza kufikiria “je, ni salama kwangu?”. Ukiliona sio salama kwako, basi binadamu mwenye akili timamu, hawezi kuacha jambo lisilo salama limuendee mwingine, lazima atachukua tahadhari yeye kwanza, kisha atatahadharisha mwingine na wengine. Haya ndio maumbile yetu. Sasa linapokuja suala la usalama wa reli nalo linaanza na mtu binafsi. Kwa hiyo, mtu unapopita kwenye njia ya reli lazima uwe makini kuzingatia alama za usalama zilizowekwa. Unapokaribia kwenye reli punguza mwendo, hakikisha hakuna treni inayokaribia eneo ulipo toka pande zote, kulia na kushoto, kabla hujaamua kuvuka reli.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Tunapohitimisha maadhimisho ya wiki hii ya Usalama wa Reli, 2023 nawasihi Wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari kwenye makutano ya reli na barabara. Aidha, nawasihi Watanzania wote tuwe walinzi wa miundombinu ya reli kwa maendeleo yetu wote. Nipende kusisitiza katika eneo hili Mhe. Raisi na Serikali yake chini ya chama cha CCM ambapo viongozi wa mkoa wapo wanatekeleza ilani kama ilivyo tajwa lakini pia kama wananchi tunatumia pesa za Nchi, na Serikali kutengeneza miundo mbinu ya reli, miundo mbinu hii ni gharama kubwa sana kwahiyo nitoe rai kwa wananchi na sisi sote kwa ujumla kutunza miundo mbinu hii kwani tunapo iharibu ndipo tunapo hatarisha pia usalama wa Usafiri wetu wa reli hivyo basi Ukiona mtu au kundi la watu linahujumu miundombinu ya reli, huo ni uhalifu, na pia ni uhujumu uchumi, kama Serikali hatuwezi kufumbia macho swala hili  toa taarifa haraka kwa mamlaka za Serikali na Jeshi la Polisi. Aidha, katika maeneo yote ambapo alama za usalama wa reli zimeondolewa, zirejeshwe upya kwa wakati ili kuimarisha usalama wa treni, abiria pamoja na mali zao.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Sote hapa ni mashahidi kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais wetu mpendwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua kwamba reli yenye usalama na ulinzi ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa nchi yetu na Afrika kwa ujumla. Hivyo, kwa utambuzi huu, Serikali imeendelea na itaendelea kuwekeza katika sekta ya usafiri wa reli kwa kutoa fedha za kujenga na kuboresha miundombinu yake ili kuwezesha uendeshaji salama wa shughuli za reli na kuhakikisha huduma zinazotolewa katika usafiri huu zinaendelea kuwa bora na salama. Lengo la kufanya haya yote ni kuhakikisha wananchi wanatumia usafiri huu salama kwa kubeba abiria na mzigo mkubwa kwa gharama nafuu huku wakijiongezea kipato kwa kusafiri na kusafirisha mazao yao na kutanua wigo wa kufanya biashara ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Tunapokamilisha maadhimisho ya Wiki hii, tunawahimiza watumiaji wa huduma za reli na wananchi wote kwa jumla wawe makini, waangalifu na wachukue tahadhari za kiusalama wakati wote wanapotumia huduma za reli wakiwa kwenye vituo vya reli, ndani ya mabehewa na hata wanapopita kwenye maeneo ya reli. Ni muhimu kufahamu kwamba treni zinakwenda kwa mwendo kasi na zinaweza kukawia au kushindwa kusimama ghafla inapotokea dharura. Aidha, nawasihi sana Watanzania msifanye shughuli za kijamii kwenye reli au pembezoni mwake kwa kuwa ni hatari na sio salama. Hivyo basi, ni wajibu wa kila mwananchi kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha na mali. Ndio maana tunasema “USALAMA UNAANZA NA WEWE, CHUKUA TAHADHARI” (“SAFETY BEGINS WITH YOUR ATTITUDE; ALWAYS BE CAREFUL”).

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Naomba nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo inakopita reli na Watanzania wote kwa ujumla, waendelee kukumbushana umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya reli pamoja na mazingira yake ili tuendelee kuboresha miundo mbinu yetu badala ya kuendelea kuboresha palepale ambapo tunajenga na wananchi wanabomoa ambapo Serikali inaendelea kupata hasara. Kwa wakandarasi na taasisi zetu sote tunapojenga miundombinu yetu tuhakikishe tunazingatia na kuboresha usalama wa wananchi. Nipende kusema machache yanayohusu sekta yetu ya reli kwa kutoa maelekezo mbalimbali.

Lakwanza ni kwa TRC, Mhe. Raisi amedhamiria kuunganisha mtandao wa reli kwa nchi nzima na kama mnavyo fahamu hivi punde tutazindua kipande kinachoanzia Tabora kwenda Kigoma. TRC ikishirikiana na Serikali tumeendeleza miradi hiyo na sasa imefikia hatua za mwisho. Nitoe maelekezo kwa TRC kuhakikisha kipande cha kwanza na cha pili kinakamilika kwa wakati, kwasababu kimesha kaa muda mrefu na wananchi hawaendelei kuweza kusubiri kwa maana mradi wa kipande cha kwanza na chapili unachelewa kukamilika, pia wana hamu ya kupanda treni kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora na kuona reli ya mwendokasi. Kwahiyo TRC muhakikishe mnamaliza kwa wakati hivi vipande viwili ambapo mpaka sasa vimefika asilimia zaidi ya 96 kukamilika.

Pili nitoe taarifa kwa wananchi kuwa Wizara kwa kushirikiana na TAZARA tupo katika hatua ya kuboresha miundombinu ya TAZARA yote haya Serikali yetu inafanya kwa madhumuni kuwa uchumi wa nchi yetu utakuwa, na wote tunafahamu sekta ndogo ya reli ni kichocheo cha uchumi lakini pia ni kichocheo kikubwa cha utoaji huduma kwani reli itasaidia usafirishaji wa mizigo hususan kutoka bandari yetu ya Dar es Salaam mpaka nchi jirani lakini pia ndani ya nchi yetu, na wananchi watakuwa wanapata huduma ya usafiri wa reli kwa raha. Kwa bahati nzuri Serikali imepitisha bajeti ya kuendeleza miundombinu hii pamoja na kuhakikisha usalama wa wananchi unaendelewa kutunzwa.    

 

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana;

Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Madhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli kwa mwaka 2023, yamefungwa rasmi.

 

NAWASHUKURU SANA KWA KUNISIKILIZA.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo