Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MHE. PROF. MAKAME M. MBARAWA (MB), WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA BODI YA WAKURUGENZI YA LATRA, JUMANNE, TAREHE 11 JULAI, 2023
11 Jul, 2023 Pakua
 • Prof. Ahmed Mohammed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA;
 • CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA;
 • Wajumbe wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya LATRA;
 • Wajumbe wa Bodi ya Kwanza ya Wakurugenzi ya LATRA mliopo;
 • Viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mliopo;
 • Menejimenti ya LATRA mliopo;
 • Ndugu wanahabari;
 • Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 

Awali ya yote, nianze kwa kumshururu Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uhai, afya njema na fursa ya kukutana hapa kwa lengo la kuzindua Bodi ya Pili ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).  Niwashukuru Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu LATRA kwa kunialika katika shughuli hii ya kuzindua Bodi ya LATRA.

 

Napenda kutumia fursa huu kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na ufuatiliaji wake wa karibu wa utendaji kazi wa Wizara na utendaji wa Taasisi za Serikali ili ziweze kutimiza vyema majukumu yake.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Leo tumekusanyika hapa kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa bodi ya pili ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA). Nitumie fursa hii kukupongeza Prof. Ahmed Mohammed Ame, kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Pili ya Wakurugenzi ya LATRA. Pia, ninawapongeza Wajumbe wote sita (6) wa Bodi hii mlioaminiwa na kuteuliwa.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Napenda mfahamu kwamba Mheshimiwa Rais aliamua kumteua Mwenyekiti mpya wa Bodi ya LATRA kutokana na sababu za kiafya za Dkt. John Ndunguru, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hii. Naomba kutumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Dkt. Ndunguru kwa mchango wake katika kuiongoza Bodi ya kwanza ya LATRA. Aidha, niwashukuru na kuwapongeza Wajumbe wa Bodi iliyopita kwa mazuri waliyoyatekeleza katika kipindi chenu.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Napenda kutumia fursa hii pia kutoa pole nyingi kwa Bodi ya iliyopita, Menejimenti ya LATRA, familia, ndugu na jamaa wa Wajumbe wawili (02) wa Bodi hiyo kwa kuondokewa na Mhandisi Leonard Kapongo aliyefariki dunia tarehe 17 Julai, 2021 na Bibi Roxana Kijazi aliyefariki dunia tarehe 24 Juni, 2022. Tutaendelea kuwakumbuka na kutambua mchango wao katika Bodi ya Kwanza ya LATRA.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Aidha, napenda kumpongeza CPA. Habibu Suluo, kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa LATRA. Serikali inayo matumaini makubwa kwako na kwamba utaendelea kutekeleza majukumu yako chini ya usimamizi wa Bodi kwa maelewano, weledi, umahiri na ufanisi.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Pamoja na mafanikio yaliyoyapatikana chini ya Bodi iliyopita lakini kulikuwa na changamoto kadhaa kutoka kwa wadau wa ndani na nje ya Taasisi. Changamoto hizo ni pamoja na Bodi kutokuisimamia vizuri Menejimenti kutekeleza majukumu yake ya kushughulikia kero za wadau wa nje na wafanyakazi wa LATRA. Mfano; hakukuwa na vikao vya mara kwa mara vya Menejimenti ya LATRA na hata vinapokuwepo, wanaoalikwa kuhudhuria sio wajumbe wote wa Menejimenti. Pia, hakukuwa na vikao vya wadau wa Sekta Binafsi na hata pale vinapofanyika hakukuwa na uwakilishi wa juu wa uongozi wa Menejimenti.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Maeneo mengine ni mapungufu katika utekelezaji wa Muundo wa Uongozi ulioidhinishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo ikiwemo ujazaji wa nafasi za uongozi katika Taasisi, uandaaji na usimamizi wa mikataba ya utendaji kazi wa watumishi (OPRAS) usio shirikishi na upandishaji wa madaraja ya wafanyakazi usio sawia, utoaji wa huduma duni kwa wateja, usimamizi hafifu wa rasilimali watu, na udhibiti usio rafiki kwa watoa huduma. Hizi ni baadhi tu ya sababu zilizotulazimu kufanya mabadiliko makubwa kuanzia kwenye Bodi na tunaendelea kwenye ngazi ya Menejimenti.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Pamoja na pongezi hizi, niwakumbushe kutimiza vyema majukumu na mamlaka yenu kama yalivyoelekezwa kwenye kifungu cha 8 na 9 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413. Jukumu kuu limetajwa katika kifungu cha 8(1) cha Sheria hiyo kuwa ni kuisimamia Menejimenti ili itekeleze vyema majukumu ya Mamlaka kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu, kupitia kwako Mwenyekiti wa Bodi, kwamba ahakikishe anashughulikia malalamiko ya wafanyakazi pamoja na wadau wa sekta ya usafiri na kuboresha huduma kwa wateja.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Katika kuisaidia Bodi hii kutekeleza vyema majukumu yake ya msingi, napenda kutumia fursa hii kuelekeza mambo mbalimbali yafuatayo yanayohitaji utekelezaji:-

 1. Kuandaa ratiba ya mwaka ya shughuli za Bodi na kuzingatia utekelezaji wake. Ratiba ijumuishe vikao vya Bodi na Kamati zake, mafunzo na ziara za Bodi kulingana na Mpango na Bajeti iliyopo;
 2. Kufanya vikao vya kawaida vya Bodi na Kamati zake kila robo mwaka na kuhakikisha Menejimenti inawasilisha taarifa za utendaji kwa wakati ili ziidhinishwe na Bodi na kuwasilishwa kwenye mamlaka husika za Serikali (Wizarani na Msajili wa Hazina);
 3. Kuzingatia nyaraka na Miongozo ya Serikali hususan zinazotolewa na Msajili wa Hazina kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bodi, stahiki za Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Katiba ya Bodi (Board Charter) na Miiko na Maadili ya Bodi (Code of Ethics and Conduct);
 4. Kuwepo na mikataba ya utendaji itakayoingiwa baina ya Bodi na Msajili wa Hazina na Baina ya Mkurugenzi Mkuu na Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi. Mikataba hiyo itekelezwe na kufanyiwa tathmini kila nusu mwaka na mwisho wa mwaka;
 5. Kusimamia mapato na matumizi ya Mamlaka na kuhakikisha mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi yanawasilishwa kwenye Mfuko wa Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizopo;
 6. Sheria na Kanuni zinazotekelezwa na Mamlaka zifahamike kwa wafanyakazi wote, wateja wenu na wadau wote wa sekta. Matumizi mazuri ya tovuti ya Mamlaka na mitandao ya kijamii (social media) ni muhimu sana wakati huu. Aidha, taarifa katika tovuti zihuishwe mara kwa mara, Maafisa habari wafanye vyema kazi ya kutoa elimu;
 7. Kufanyia mapitio Muundo wa Uongozi uliopo, kuwasiliana na Msajili wa Hazina na Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora ili kuhakikisha Muundo unaendana na majukumu ya LATRA. Mfano, eneo la Usafiri wa Waya (Cable Transport) ni jukumu la msingi la Mamlaka lakini halipo kwenye Muundo wa sasa. Tujiridhishe pia endapo Muundo huo unaendana na uwekezaji mkubwa wa Serikali kwenye reli ya kisasa (SGR);
 8. Kupitia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na kuhakikisha hakuna mgongano wa kisheria au wa kimaslahi baina ya LATRA na Taasisi nyingine za umma. Mfano; Sheria za Jeshi la Polisi na Mamlaka za Halmashauri;
 9. Kushirikiana na Wizara katika utayarishaji na uboreshaji wa Kanuni za Mamlaka. Aidha, Wadau wa mamlaka, hususan sekta binafsi, washirikishwe kikamilifu kabla ya Mamlaka kufanya maamuzi yanayoathiri utoaji wa huduma mnazodhibiti. Tusifanye maamuzi ya kushtukiza na kuwakwaza wadau wetu, lazima wajue kesho yao ili nao waweke mipango yao vizuri;
 10. Kuweka utaratibu wa Mamlaka kukutana na wadau wake kila mwaka na kutoa elimu juu ya shughuli za Mamlaka. Elimu itolewe pia kwa wateja wote wa Mamlaka kupitia njia mbalimbali na kuwe na programu inayofahamika ya kutoa elimu kwa umma kuhusu LATRA, majukumu yake, haki za watumiaji na watoa huduma;

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;

Mambo mengine ya kuzingatia na kutekeleza ni:

11. Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) zijibiwe kwa wakati na mapendekezo yote yaliyotolewa na CAG yatekelezwe kwa asilimia 100. Taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya CAG iwasilishwe kwa Katibu Mkuu (Uchukuzi). Aidha, muwe na mkakati wa kupunguza au kuondoa kabisa Hoja za ukaguzi wa ndani na nje;

12. Kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa kisekta yanayotekelezwa na Mamlaka kwenye eneo la usafiri wa ardhini baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ);

13. Kuzingatia Sheria na Kanuni za Manunuzi ya Umma katika manunuzi yote na uondoshaji wa bidhaa chakavu (disposal). Hii ni pamoja na kuhakikisha matumizi ya mfumo wa manunuzi ya umma (TANePS uliopo au NeST unaojengwa) unafahamika na kutumika kama unavyoelekezwa na PPRA; Kushauri Wizara kuhusu utaratibu wa mabasi yanayokwenda mikoani kufanya safari kwa saa 24 na kusimamia kwa umakini mkubwa utaratibu utakaowekwa katika kuruhusu mabasi hayo kusafiri kwa ratiba za saa 24. Hatua hii inafuatia uamuzi wa Serikali wa kuruhusu mabasi kufanya safari usiku kama ilivyo tamkwa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa tarehe 28 Juni, 2023;

14. Kushirikiana na Wizara kuhakikisha rasimu ya Kanuni zilizowasilishwa kwa wadau, hususan za Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) na Mfumo wa Tiketi Mtandao (E-Ticketing) vinakamilika kwa haraka. Aidha, changamoto zote katika matumizi ya mifumo hiyo ipatiwe ufumbuzi mapema;

15. Kuboresha Mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za ndani na nje ya Mamlaka. Nasisitiza, mharakishe maboresho ya Mfumo wa Utoaji Leseni (RRIMS) unatekelezwa na kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA);

16. Kuweka mikakati madhubuti ya udhibiti wa huduma za usafiri kwa njia ya barabara na reli na kuhakikisha zinakuwa salama ili kuepuka matukio ya mara kwa mara ya ajali. Eneo hili lipewe kipaumbele kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama;

17. Kusimamia kwa karibu na kuhakikisha upatikanaji wa usafiri wa uhakika wa mabasi yaendayo haraka (DART) na usafiri wa treni za abiria pia kuhakikisha tiketi za safari zinapatikana kwa njia ya mtandao (kielekroniki) au kwa matumizi ya kadi ili kuondoa upotevu wa mapato ya Serikali na foleni zinazopotezea abiria muda; na

18. Kuzingatia misingi ya utawala bora na mipaka ya utendaji. Jukumu kubwa la Bodi ni kuisimamia Menejimenti, sio kufanya kazi za Menejimenti. Bodi ipate mafunzo ya kutosha (Induction Program) na kufanya ziara za kujifunza ili kutekeleza vyema majukumu yake.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Kwa maagizo haya, ni matumaini yangu kuwa Bodi hii itatekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria na Miongozo ya iliyopo ili kukidhi matarajio ya Serikali na wananchi kwa ujumla.

 

Bodi hii inatarajiwa kufanya kazi kubwa na nzuri zaidi hususan katika kutekeleza misingi ya utawala bora, kuweka mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi, kuboresha usafiri wa abiria na mizigo, kujenga mahusiano mema na chanya na wadau wa Mamlaka na kuhakikisha usimamizi  borawa rasilimali za umma kama inavyosisitizwa na Mheshimkiwa. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, Bodi hii inayo kazi kubwa ya kutekeleza majukumu yake.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe,

Baada ya kusema haya, napenda kutamka kuwa Bodi ya Pili ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini imezinduliwa rasmi, na sasa nipo tayari kuwakabidhi Mwenyekiti wa Bodi na Wajumbe wa Bodi vitendea kazi kwa ajili ya  kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

 

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo