Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU (LATRA) KATIKA HAFLA YA UTOAJI WA VYETI KWA MADEREVA WA VYOMBO VYA MOTO VINAVYOTOA HUDUMA YA USAFIRI KIBIASHARA WALIOFANYA MTIHANI NA KUTHIBITISHWA.
01 Jul, 2023 Pakua
 • Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete (Mb), Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi),
 • Mhe. Jumanne Sagine (Mb), Naibu Waziri Mambo ya Ndani na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,
 • Dkt. Zainab Rashid, Mwenyekiti wa Kamati ya Uthibitishaji Madereva-LATRA,
 • Ndugu Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Serikali mliopo hapa,
 • Ndugu Wenyeviti na Viongozi wa Vyama vya Madereva na Wasafirishaji ikiwemo CHAWAMATA, TADWU, UWAMATA, TATOA, TAT, TAMSTOA, TRFA, DARCOBOA na UWADAR,
 • Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa,
 • Ndugu wanahabari,
 • Wageni waalikwa mabibi na mabwana, Itifaki imezingatiwa,

 

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Nianze kwa kumshururu Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uhai, afya njema na fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuwatambua, kuwapongeza na kuwatunuku vyeti madereva 999 waliofanya mitiahani ya kuthibitishwa na kufaulu.

Pili, naomba nitoe shukrani za moyoni na za kipekee kwako Mhe. Naibu Waziri (Sekta ya Uchukuzi) kwa kukubali ombi letu la kuwa Mgeni Rasmi kwenye hafla hii muhimu katika eneo letu la udhibiti. Tunafahamu kuwa unayo majukumu mengi na mazito lakini umeweza kuipa thamani hafla hii kwa kutenga muda wako ili kujumuika nasi. Tunakushukuru sana.

Tatu, kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa LATRA, natumia fursa hii kumpongeza sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na miongozo mizuri inayotuwezesha kutekeleza vyema majukumu yetu ya kuwatumikia watanzania na pia kuendelea kuishirikisha sekta binafsi katika utoajia wa huduma tunazosimamia. Hapa hatuna budi kutoa shukrani nyingi sana kwa viongozi wa Wizara yetu kwa namna wanavyotuongoza, hususan Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (Mb), Naibu Waziri Wizara ya 3 Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) na Bw. Gabriel Migire, Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) na Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi.

Nne, na kwa umuhimu mkubwa, natumia fursa hii pia kutoa shukrani maalum kwa madereva waliofanya mitihani ya kuthibitishwa na LATRA na kipekee nawapongeza wote waliofaulu na kustahili kupewa vyeti vya kuthibitishwa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

LATRA ni mdhibiti wa usafiri ardhini wenye maoneo makuu matatu- usafiri wa barabara (road transport), usafiri wa reli (railways transport) na usafiri wa waya (cable transport). Kwa ufupi, majukumu ya LATRA kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, yametajwa katika kifungu cha (5)(1) ikijumuisha:

 1. Kutekeleza majukumu ya sheria za kisekta;
 2. Kutoa, kuhuisha, au kufuta leseni;
 3. Kwa mujibu wa sheria za kisekta:
  • Kusimamia viwango  vya ubora wa huduma  na usalama katika sekta zinazosimamiwa
  • Kusimamia viwango na masharti ya utoaji wa huduma zinazodhibitiwa
  • Kudhibiti viwango vya tozo za huduma
 4. Kuratibu shughuli za usalama wa usafiri wa ardhini;
 5. Kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa sekta zinazodhibitiwa;
 6. Kuhakikisha kuwa treni na magari ya abiria yana ubora unaotakiwa;
 7. Kufuatilia mwenendo wa utendaji kazi wa sekta zinazodhibitiwa kwa kuangalia kiwango cha uwekezaji, gharama za kutoa huduma, ufanisi na ueneaji wa huduma;
 8. Kuwezesha utatuzi wa migogoro na malalamiko; na
 9. Kuelimisha umma kuhusu kazi na wajibu wa Mamlaka

Leo tunatekeleza kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya LATRA iliyotupa jukumu la Kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa sekta zinazodhibitiwa (vyombo vya usafiri wa kibiashara na treni). Hivyo, kwetu ni siku muhimu sana na ya kihistoria kwa kuwa tunashuhudia moja katika mafanikio yetu katika kutekeleza Sheria na Kanuni tulizokabidhiwa na Serikali ili kuzitekeleza.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Ili kutekeleza kazi ya Kusajili Wahudumu na Kuthibitisha Madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara Mhe. Waziri 5 mwenye dhamana ya uchukuzi aliidhinisha Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili wa Wahudumu wa Vyombo vya Moto Kibiashara zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 81 la tarehe 7 Januari, 2020. 

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Vilevile, wazo la Mamlaka kutahini madereva lilitokana na ushauri uliotolewa katika Sera ya Taifa ya Usalama Barabarani ya Mwaka 2009 ambayo imeainisha juhudi mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ili kupunguza ajali za barabarani nchini. Tafiti zinaonesha ajali nyingi za barabarani na usafiri wa reli kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na makosa ya kibinadamu. Somo la kupunguza ajali nchini linaloonekana katika Sera hiyo ni kukabiliana na masuala ya usalama kwa kutumia mifumo itakayochangia katika kuleta mabadiliko ya tabia za madereva nchini.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kufuatia njia hiyo iliyoainishwa kwenye Sera, na kuwepo kwa Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili wa Wahudumu wa Vyombo vya Moto Kibiashara, mwezi Disemba, 2020 Mamlaka ilianza rasmi kusajili madereva kwa lengo la kuwathibitisha. Kufikia mwezi Mei, 2020, LATRA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ilikamilisha utengenezaji na usimikaji Mfumo wa Kutahini Madereva (Drivers Testing 6 System) wa magari yanayotoa huduma kibiashara. Kwa kutumia mfumo huo, dereva anafanya mtihani kwa njia ya kompyuta na baada ya kuwasilisha mtihani wake, unasahihishwa kieletroni na kupeleka matokeo ya mtihani kwa dereva husika kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno – SMS.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Kabla ya kuanza kutahini madereva, Mamlaka kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ilipitia maswali ya mtihani yanayotumika kwenye vyuo vinavyozalisha madereva nchini kulingana na mitaala inayotumika na kuyaweka katika mfumo wa DTS. Maswali hayo yanawapima madereva kuhusu uelewa wao kwenye maeneo ya alama na miongozo mbalimbali inayowasaidia kuendesha vyombo vya moto kwa usalama.

 

Aidha, baada ya maswali kupitishwa na kuwekwa kwenye mfumo, tarehe 1 Juni, 2022 Mamlaka ilianza rasmi kutumia mfumo wa DTS kutahini madereva ambapo hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2023 jumla ya madereva 1,744 walikuwa wamefanya mtihani na madereva 999 walifaulu, ambao baadhi yao utawapatia vyeti vya kuthibitishwa katika hafla hii.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kwa kuwa tunawajali madereva wetu na tunataka wafaulu kwa wingi, LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, tumeandaa video mbalimbali zinazoelimisha kuhusu masuala ya msingi ya kuzingatia ukiwa barabarani ikiwemo suala la alama. Video hizi zinapatikana katika Online TV ya Mamlaka inayopatikana kwa jina la LatraTV kwenye mtandao wa YouTube.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Mchakato wa utoaji wa vyeti vya uthibitishaji wa madereva unaratibiwa na Kamati ya Uthibitishaji (Certification Committee) yenye wajumbe watano (5) wanaoteuliwa na Mamlaka kwa mujibu wa kanuni ya 6(1) ya Kanuni za LATRA za Uthibitishaji wa Madereva na Usajili Wahudumu Magari ya Biashara za mwaka 2020. Hivyo, Mamlaka iliunda Kamati ya Uthibitishaji madereva yenye wajumbe watano ambayo Mwenyekiti wake ni Dr Zainabu Rashid na Makamu wake ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mstaafu na Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Bw. Mohamed Mpinga. Wajumbe wengine ni Bw. Hans Tomas Mwaipopo, Bw. Venance Adamsom Mwanyumba na Mjumbe mmoja toka Jeshi la PolisiKikosi cha Usalama Barabarani. Uteuzi wa Wajumbe hawa ni kwa kipindi 8 cha miaka mitatu (3) kwa mujibu wa kanuni ya 6(2) ya GN 81 na wanaweza kuteuliwa kwa kipindi kingine kimoja tu.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Moja ya masharti ya leseni zinazotolewa na LATRA ni wenye vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara, kuhakikisha kila dereva anayeendesha vyombo hivyo ana Cheti cha Uthibitisho kinachotolewa na Mamlaka baada ya kufanya mtihani wa kuthibitishwa na kufaulu. Sharti la leseni kwa mtoa huduma za usafiri wa abiria kutumia dereva mwenye cheti cha uthibitisho kinachotolewa na Mamlaka, limeainishwa kwenye Kanuni ya 22(i) ya Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria), 2020. Kanuni ya 22(e) pia inaelekeza dereva haruhusiwi kuendesha gari kwa zaidi ya saa 8 mfululizo.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kuna faida nyingi za madereva kuthibitishwa, naomba nizitaje chache;

(i)Kurasmisha fani ya udereva ili iheshimike kama zilivyo fani zingine;

(ii) Kuwezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazo wezesha kusimamia maslahi ya madereva katika ajira;

(iii) Kuwawezesha madereva kutambulika rasmi kikanda na kimataifa;

(iv) Kuongeza nidhamu na uwajibikaji kwa madereva; na

(v) Kuboresha uchunguzi wa matukio ya ajali zinapotokea.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Sambamba na kuthibitisha madereva, Sheria ya LATRA imetupatia jukumu la kusajili wahudumu wa vyombo tunavyovidhibiti. Ili kutekeleza jukumu la kusajili wahudumu magari ya kibiashara, Mamlaka kwa kushirikiana na Vyama vya Wamiliki wa Mabasi (TABOA na DARCOBOA) na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji nchini tulitengeneza mwongozo wa uandaaji mitaala itakayotumika kutoa mafunzo kwa kundi hilo kwa kuzingatia mahitaji ya kisheria, mahitaji ya jamii na watoa huduma za usafiri nchini. Mwongozo huo utatumiwa na vyuo washirika katika kuandaa mitaala ya mafunzo ya wahudumu. Leo utaizindua rasmi mitaala ilioandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Biashara (CBE) ili vyuo hivyo vianze kutoa mafunzo kwa kundi linalokusudiwa na baadae Mamlaka ikamilishe jukumu la kuwasajili wahudumu wa magari ya kibiashara na kutoa vitambulisho kwa mujibu wa Kanuni. Nawapongeza sana wakuu wa vyuo hivi viwili pamoja na Menejimenti zao kwa kazi hii kubwa yaliyoifanya kwa maslahi mapana ya Taifa na sekta yetu ya Uchukuzi. Hizi zimekuwa taasisi za mwanzo kabisa kuandaa mitaala kwenye eneo hili jipya la udhibiti kwa Mamlaka yetu. Honera sana.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Naomba nitumie fursa hii kutoa rai kwa madereva na wamiliki wa magari ya kukodiwa kwa safari maalum (Special Hire) ambao wanaingilia huduma za mabasi ya masafa marefu; kuanzia leo tarehe 1 Julai, 2023 mtoa huduma yeyote wa Special Hire kufanya safari kinyume na masharti ya leseni yake, tutaifuta leseni hiyo na takuwa huru kuomba leseni za huduma nyingine (kama daladala). Aidha, niwatake madereva wote ambao wameshasajiliwa kwenye mfumo wa VTS na kupatiwa kifaa cha utambulisho (i-button), wahakikishe wanatumia kifaa hicho kila wanapoendesha mabasi.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Nimalizie hotuba yangu kwa kujibu swali moja ambalo nimeulizwa sana na wanahabari baada ya Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kueleza ruhusa ya Serikali kwa mabasi kusafiri saa 24 wakati akiahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 28 Juni, 2023.

Ninanukuu:

‘Usafiri wa mabasi ya Mikoani

38. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mwishoni mwa miaka ya 1990 Serikali ilizuia mabasi ya abiria kusafiri usiku. Zuio hilo lilisababishwa na matukio ya utekaji wa mabasi uliohusisha uporaji na udhalilishaji wa abiria, ajali mbaya za mabasi zilizogharimu Maisha ya watu na wengine kupata ulemavu wa kudumu na uharibifu wa mali na miundombinu ya barabara. Utekaji wa mabasi ulikuwa unafanyika kwenye maeneo yaliyokuwa na barabara mbovu na ambayo hayakuwa na mawasiliano ya simu.

39. Mheshimiwa Spika,

sote ni mashahidi kuwa changamoto za usalama na miundombinu zilizokuwepo kipindi hicho zimepungua kwa kiasi kikubwa au kuondolewa kabisa kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Miundombinu ya barabara na mawasiliano ya simu vimeimarishwa karibu maeneo yote nchini. Aidha, juhudi za Jeshi la Polisi katika kupambana na kudhibiti uhalifu ikiwemo kufanya doria katika barabara kuu na barabara za Mikoa na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) kuanza kutekeleza mfumo wa ufuatiliaji mwendo wa mabasi ya abiria (VTS) vimesaidia kupunguza matukio makubwa ya ajali za barabarani.

40. Mheshimiwa Spika,

 kufuatia mabadiliko hayo chanya na maoni ya wadau mbalimbali wa usafiri na usafirishaji wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, utayari wa wamiliki na madereva wa mabasi kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, utayari wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuimarisha doria, Serikali imeamua kuondoa zuio la 12 mabasi ya abiria kusafiri nyakati za usiku lililowekwa miaka ya 1990. Ili kutekeleza uamuzi huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itashirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hususan sekta ya Uchukuzi kuweka utaratibu utakaofuatwa na wamiliki na madereva wa mabasi ya abiria wenye nia ya kusafirisha abiria nyakati za usiku.” (Mwisho wa Kunukuu)

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kufuatia maelekezo haya ya Serikali yaliyotolewa na Mhe. Waziri Mkuu, LATRA itakuwa tayari kusimamia utaratibu utakaowekwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hususan sekta ya Uchukuzi ili ufuatwe na wamiliki na madereva wa mabasi ya abiria wenye nia ya kusafirisha abiria nyakati za usiku. LATRA iko tayari kusubiri maelekezo ya Wizara

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inaandaa Kanuni za Usimamizi wa Mfumo wa Kufuatilia Mwendendo wa Magari (VTS Regulations). Kanuni hii ni nyenzo muhimu ya udhibiti wa VTS na washiriki wote (wamiliki, madereva, vendors).

VTS Standard – TZS 3172:2021 ilishatolewa na Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) na kutangazwa katika Gazeti la Serikali (GN), Tangazo Na. 164 la tarehe 10 Machi, 2023.

Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima naomba nikukaribishe uongee na hadhara hii, kisha nakuomba utekeleze jukumu kubwa la kufungua hafla hii uzinduzi wa mtaala utakaotumika kutoa mafunzo kwa wahudumu wa magari ya kibiashara na utoaji wa vyeti kwa madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma ya usafiri kibiashara.

 

Asanteni kwa kunisikiliza

 

CPA Habibu J. Suluo

Mkurugenzi Mkuu LATRA

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo