Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU (LATRA) KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA WADAU KUHUSU MATUMIZI YA TEKSIMITA KWA MAGARI YA KUKODI (CONVECTIONAL TAXI) DESEMBA 14, 2022
14 Dec, 2022 Pakua

Mheshimiwa Amos Makala, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,

Ndugu Wakuu na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali,

Ndugu Dkt. Alhaji Fimbo,  Mwenyekiti wa mkutano wa wadau,

Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa,

Ndugu wanahabari,

Wageni waalika mabibi na mabwana

NINAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA!      KAZI - IENDELEE !!!

 

Awali ya yote natoa shukrani za kipekee kwako Mgeni rasmi kwa kukubali ombi letu na kujumuika nasi katika mkutano huu wa kuwasilisha kwenu takwa la kisheria la matumizi ya mita za teksi kwa ajili ya kukokotoa nauli kwa magari yanayotoa huduma ya usafiri wa kukodi.

 Tunafahamu kuwa unayo majukumu mengi na makubwa yenye maslahi makubwa kwa Taifa, hata hivyo umeweza kutenga muda na kufika hapa ili kutimiza jukumu hili ambalo pia ni la maslahi makubwa kwa Watanzania na Taifa letu kwa jumla.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Jukumu tunalolifanya hapa leo hii ni kwa mujibu wa Sheria ya LATRA na. 3 ya mwaka 2019 na kanuni ya 15 (d) ya LATRA ya Usafiri wa Kukodi ya mwaka 2020. Kanuni ya 15(d) kinaelekeza kuwa vyombo vyote vinavyopewa leseni ya usafiri wa kukodi vinatakiwa kuwa na mita ya nauli au mfumo unaweza kukukotoa nauli. Jukumu hili la ushirikishaji umma ni zao la utawala bora ambapo inasisitizwa kushirikisha wadau kwenye utekelezji wa majukumu ya kiudhibiti ambayo misingi yake imejengwa kwenye Sheria ya LATRA ya mwaka 2019 na kanuni zake..

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Mkutano wetu wa leo utakuwa na mawasilisho kutoka kwa  mdhibiti  kuhusu utekeleazji wa kanuni ya magari ya kukodi kifungu 15(d). Aidha, Shirika letu la Viwango TBS litapata nafasi ya kutushirikisha kuhusu viwango vinavyotakiwa kwa mita za teksi hapa nchini ambavyo havitofautiani na nchi zingine. Vilevile, LATRA CCC nao watapata nafasi ya kuwasemea watumiaji wa huduma tunazodhibiti.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Natoa shukrani za dhati kwa wadau wote waliopo hapa kwa kukubali mwaliko wetu na kuhudhuria mkutano huu. Ninatambua kila mmoja wetu ana majukumu mazito ya kiofisi au binafsi lakini kwa kutambua umuhimu wa mkutano huu ameacha shughuli zake ili kwa pamoja tuweze kushirikiana. Napenda kusema kwa msisitizo kuwa mkutano huu ni kwa ajili yenu ndugu wadau hivyo mnaombwa kufuatilia kwa umakini na kisha mtoe maoni yenu kwa uhuru.

Niwahakikishie kuwa mchango wa kila mmoja wenu hapa ni wa muhimu sana na watalaam wetu hapa watanakili maoni ya kila mtu kisha kufanya uchambuzi wa kina ili  kuiwezesha Mamlaka kufanya uamuzi kwa kuzingatia maoni ya wadau.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

LATRA, kwa kutambua ukweli kwamba si wadau wote wangeweza kufika hapa, tumeweka utaratibu wa kuendelea kupokea maoni kwa njia ya maandishi hadi tarehe 31 mwezi Desemba mwaka huu. Maoni hayo yanaweza wasilishwa kwa kufikishwa katika ofisi zetu zilizopo mikoa yote au kwa barua pepe ambayo ni dg@latra.go.tz

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima naomba nikukaribishe uongee na hadhara hii, kisha nakuomba utekeleze jukumu kubwa la kufungua mkutano wa wadau wetu kuhusu matumizi ya mita za teksi  kwa ajili ya huduma ya usafiri wa kukodi kwa maslahi ya watoa huduma na wananchi wote wanaotumia huduma za usafiri huo.

Asanteni kwa kunisikiliza

 

Johansen Kahatano.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu LATRA

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo