Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM MHE. AMOS MALAKA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA WADAU WA KUPOKEA MAONI KUHUSU UTARATIBU WA MATUMIZI YA TEKSIMITA DESEMBA 14, 2022
14 Dec, 2022 Pakua

Ndugu Johansen Kahatano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,

Ndugu Alhaj Juma Fimbo, Mwenyekiti wa Mkutano wa Wadau,

Ndugu Wakuu na wawakilishi wa Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali,

Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa,

Ndugu wanahabari,

Wageni waalikwa mabibi na mabwana,

NINAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA! KAZI - IENDELEE !!!

 

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai na kuibariki Serikali yetu, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia nashukuru kwa heshima niliyopewa na LATRA ya kuwa mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mkutano huu unaolenga kupokea maoni ya wadau kuhusu utaratibu wa matumizi wa mita za  teksi (taximeter) kwenye usafiri wa teksi za kawaida ambazo hutumika kwa kukodishwa kwa safari binafsi hapa nchini. Matumizi ya teksimita yatasaidia kukokotoa kiwango cha nauli atakachotakiwa kulipa mteja baaada ya kufika mwisho wa safari.

Ndugu wageni waalikwa,

Kabla ya kuongea zaidi kuhusu mkutano huu wa leo, naomba niseme yafuatayo kwa ufupi kabisa, Sote ni mashahidi kuwa Serikali ya awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya juhudi za kipekee kuhakikisha inakuza sekta binafsi kwa kuhakikisha sekta binafsi ndio inakuwa chachu ya kusukuma uchumi na chanzo cha mapato ya serikali kupitia kodi na kuongeza ajira kwa vijana hasa kwenye huduma za usafiri aridhini ikihusisha magari ya kukodi na huduma za usafiri wa mijini kwa kutumia mabasi na pikipiki za miguu miwili na mitatu.

Aidha, kuimarika kwa miundombinu ya barabara katika maeneo mengi hapa nchini imesaidia kuimarika kwa usalama na ubora wa huduma za  usafiri wa barabara na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji uchumi.

Ndugu wageni waalikwa,

Jukumu letu la leo ni kupokea maoni na kujadili kuhusu utaratibu wa matumizi ya mita za  teksi (taximeter) kwenye usafiri wa teksi za kawaida. Jukumu hili tunalolifanya ni kwa mujibu wa Sheria ya LATRA ya mwaka 2019 na kanuni namba 15(d), ya Kanuni za Usafiri wa Kukodi za LATRA za mwaka 2020. Hivyo nawasihi kila mmoja wetu, kwa kuzingatia umuhimu wa kazi hii atimize wajibu wake kwa umahiri na utulivu wa hali ya juu.

Pia, nimefurahi kusikia Mkurugenzi Mkuu wa LATRA amesema kuwa wadau ambao hawakuweza kufika hapa wanaweza kuendelea kuwasilisha maoni yao kwa maandishi hadi tarehe 31 mwezi Desemba mwaka huu.

Natoa rai kwa wadau mbalimbali kuitumia vizuri nafasi hii, ili kuwawezesha wataalam wetu kufanya kazi yao kwa ufanisi ili Tanzania iwe mfano wa kuigwa na nchi zingine na waje kujifunza kwetu namna bora ya kusimamia huduma za usafiri ardhini.

 

 

Ndugu wageni waalikwa,

Kwa kuwa mkutano huu ni wa kwenu kujadili na kutoa maoni, mimi kazi yangu ni kufungua mkutano huu.

Kwa hayo machache, napenda kutamka rasmi kuwa mkutano wa wadau wa kupokea na kujadili matumizi ya mita za teksi kwenye usafiri wa magari ya kukodi hususani taksi za kawaida umefunguliwa Rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza

 

Amosi Makalla

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam

 

 

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo