Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu Uchukuzi,
Ndugu Benjamin Mbimbi, Mkurugenzi Msaidizi Usafiri wa Reli kutoka Wizara ya Uchukuzi,
Ndugu Damas A. Mwajanga, Mkuu wa Chuo cha Reli – Tabora, Unayemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu TRC,
Wawakilishi wa taasisi mbalimbali,
Wadau wote wa usafiri wa reli mlioko hapa,
Ndugu Wanahabari, Mabibi na Mabwana,
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA……
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Napenda kuanza kwa kumshurkuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, kwa kutuwezesha kukusanyika hapa leo hii, kukamilisha maadhimisho haya ya wiki ya usalama wa reli yenye kaulimbiu ya Usalama unaanza na wewe, chukua tahadhari. Pia natoa shukrani za kipekee kwako Mgeni rasmi kwa kukubali ombi letu na kujumuika nasi katika shughuli hii muhimu ya kufunga maadhimisho ya wiki ya usalama wa reli katika viwanja hivi vya Chuo cha Teknolojia ya Reli hapa Mkoani Tabora. Tunafahamu kuwa unayo majukumu mengi na makubwa yenye maslahi makubwa kwa Taifa, hata hivyo umeweza kutenga muda Kusafiri na kufika hapa ili kutimiza jukumu hili ambalo pia ni la maslahi makubwa kitaifa na kimataifa katika maendeleo ya sekta ya reli.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Jukumu la kuadhimisha wiki ya usalama wa reli ni kwa mujibu wa itifaki ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo Tanzania ni nchi mwanachama, hivyo, maadhimisho haya yanafanyika katika Nchi Wanachama wa Reli Kusini mwa Africa (SARA).
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Maadhisho yetu yamefanyika wiki hii kuanzia Jumatatu tarehe 09 Oktoba, 2023 ambapo tumekuwa na maonesho ya taasisi mbalimbali ambayo umeyashuhudia ulipotembelea mabanda ya maonesho. Aidha tumekuwa na kampeni za kuwafikia wadau zilizofanyika siku zote za maadhimisho haya. Kampeni hizo zilihusisasha utoaji wa elimu ya usalama wa reli kwa wadau tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na mashuleni, kuwafikia wakazi wa maeneo yaliyopo jirani na miundombinu ya reli, maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Aidha, kampeni hizo zilizolenga kuongeza uelewa na tahadhari za usalama wa reli kwa wananchi zimefanyika katika Nchi zote wanachama wa SARA ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunatoa shukrani za dhati kwa mapokezi na ukarimu tulioupata kutoka kwa wenyeji wetu wa mkoa huu wakiongozwa na Mheshimiwa, Balozi, Dkt. Batilda Buriani, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Wakuu wa Wilaya zote mkoani hapa bila kumsahau Mheshimiwa Zakaria Mwansasu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, ambaye alitufungulia maadhimisho haya siku ya Jumatatu yarehe 09 Oktoba, 2023.
Tunatoa shukrani za dhati kwa wadau wengine wote waliotupa ushirikiano uliopelekea kufanikisha maadhimisho haya bila kumsahau Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora.
Shukrani hizi ziwafikieni wadau wote mliopo hapa kwa kukubali mwaliko wetu na kuhudhuria mkutano huu. Tunatambua kila mmoja wetu ana majukumu mazito ya kiofisi au binafsi lakini kwa kutambua umuhimu wa maadhimisho haya, ameacha shughuli zake ili kwa pamoja tuweze kushirikiana.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kwetu kama wadhibiti wa kiuchumi na kiusalama tunatambua nafasi yetu katika kuhakikisha usalama wa reli unapewa nafasi inayostahili. Hii ni pamoja na kusimamia viwango katika ujenzi wa miundombinu na uendeshaji wa huduma. Na hapa tunapata faida kubwa ya kushirikiana na wanachama wenzetu wa SARA ambao wamepiga hatua zaidi katika udhibiti na kutoa huduma za usafiri wa reli.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunatoa shukrani za kipekee kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwezesha ujenzi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa reli unaondelea na kuboresha miundombinu ya reli iliyopo. Kwa hakika, sisi sote kama wadau tunapaswa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kuzingatia usalama reli na kutekeleza masuala mbalimbali yatakayoongeza tija katika matumizi ya miundombinu ya reli.
Aidha, tunamshukuru kwa dhati Mheshimiwa Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, kwa kuwa yeye amejipambanua katika kusimamia usalama wa reli hapa nchini ambapo hata wiki iliyopita alikuwa hapa na wiki hii ya maadhimisho aliendelea kukagua huduma za reli kwa njia za Mpanda na Kigoma, alkiongea na uongozi wa TRC na wafanyakazi wanaotoa huduma moja kwa moja (Critical Safety Workers) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha reli zetu zinafanya kazi kwa usalama na kwa ufanisi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunaendelea kuwakumbusha waendeshaji wa huduma za reli nchini ambao ni Shirika la Reli Nchini (TRC) na Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa huduma za reli ili kuhakikisha usalama na kutoa huduma kwa ufanisi ikiwemo treni kufika vituoni kwa wakati.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunaendelea kusisitiza juu ya matumizi ya mifumo katika kuongeza ufanisi, hii ni pamoja na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na Mfumo wa Tiketi Mtandao ili kuongeza usalama na kuhakikisha ufanisi wa kiuchumi katika reli zetu. Yote haya yanawezekana iwapo tutaamua kubadilika.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunapoelekea kufunga maadhimisho haya ya wiki ya Usalama wa Reli, yenye kaulimbiu ya Usalama Unaanza na wewe, chukua tahadhari, nawasihi Wananchi wote na madereva wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari endelevu wanapotumia miundombinu ya reli. Tunaamini kuwa mwisho wa maadhimisho haya sio mwisho wa tahadhari za usalama, bali ni muendelezo wa kuzingatia usalama ili mwaka ujao tuadhimishe tukiwa na fuhara ya mafanikio yaliyotokana na maadhimisho yam waka huu. Kila mmoja wetu awe mlinzi wa miundombinu ya reli kwa maendeleo ya Nchi yetu.
Baada ya kusema hayo, naomba niishie hapa ili nitoe fursa kwa ratiba ya shughuli hii kuendelea.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.