Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

Hotuba ya Mkurugenzi Mkuu LATRA Bw. Gilliard W. Ngewe wakati wa Mkutano wa Wadau Mei 26, 2022
26 May, 2022 Pakua
 • Ndugu Mgeni Rasmi, Dkt. Charles Enock Msonde, Mhe. Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI,
 • Dkt. Edwin Mhede, Mkurugenzi Mkuu DART,
 • Ndugu Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini,
 • Ndugu Wakuu na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali,
 • Ndugu watumishi wa DART, LATRA NA UDA-RT
 • Chama cha Kutetea Abiria,
 • Ndugu wasafirishaji na wadau mbalimbali mliojumuika hapa
 • Ndugu wanahabari,
 • Wageni waalikwa mabibi na mabwana,

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya na kuendelea kuibariki Serikali yetu, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, natoa shukrani za kipekee kwako mheshimiwa mgeni Rasmi kwa kukubali mualiko wetu, tunajua unayo majukumu mengi muhimu ya kujenga Taifa, lakini umeweza kutenga muda kwa ajili ya mkutano wetu huu.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Tarehe 18 Mei mwaka 2022, Mamlaka ilipokea maombi ya mapendekezo ya nauli mpya kwa wasafiri wanaotumia mabasi yaendayo haraka kutoka kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka – DART.

Sheria ya LATRA Na. 3 ya Mwaka 2019, Kifungu Na. 21 Sura ya 413, inaitaka Mamlaka pindi inapopokea maombi kutoka kwa watoa huduma, kuitisha kikao cha pamoja kwa ajili ya majadiliano kuhusu mapendekezo kama yalivyotolewa na Wakala.

Hivyo, kwa kuzingatia hilo, tarehe 19 Mei, tulitoa taarifa kwa umma inayowaalika wadau wote katika mkutano huu ili tuwasikilize na kukusanya maoni kabla ya kufikia uamuzi kuhusu viwango vya nauli vinavyopendekezwa,na kwa kazi hiyo leo hii tuko hapa.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Sote tunafahamu kuwa moja kati ya misingi ya utawala bora ni ushirikishwaji, nami nawasihi wadau kuitumia nafasi hii kujadili kwa kina huku tukizingatia gharama za uendeshaji na maisha halisi ya mtanzania, lengo ni kuwa watumia huduma na watoa huduma wote shirikishwe katika kufikia maamuzi na hatimaye maamuzi yatakayofikiwa yawe na tija na uhalisia kwa wote.

Aidha, sote tukumbuke kuwa huduma ya usafiri ikiwemo huduma ya usafiri mijini tunayoijadili leo hii ni huduma ya lazima katika jamii. Hivyo napenda kutoa wito kwenu wadau tuwe mabalozi wa dhati, katika kujadili kwa hoja zenye mashiko bila jazba.

Kila mmoja aliyefanikiwa kufika hapa ajuwe kuwa kuna watu wengi anaowawakilisha, hivyo kila mmoja wetu ajitahidi kuwawakilisha ipasavyo.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Kwa kuwa jukumu hili tunalofanya leo hii ni kwa mujibu wa Sheria, nawasihi kila mmoja wetu, kwa kuzingatia umuhimu wa kazi hii atimize wajibu wake kwa umahiri na utulivu wa hali ya juu.

Vilevile, kwa wadau ambao wangependa kuwasilisha maoni yao kwa maandishi wanayo nafasi ya kuwasilisha maoni yao kwa maandishi katika Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu iliyopo katika Jengo la Mamlaka, Barabara ya Nkrumah kabla ya tarehe 07 Juni, 2022. Pia, maoni yanaweza kutumwa kwa barua pepe kupitia anuani hizi: info@latra.go.tz na dg@latra.go.tz

Natoa wito kwa wadau mbalimbali kuitumia vizuri nafasi hii, ili kuwawezesha wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi na ueledi wa hali ya juu.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha kuwa, katika kazi ya kupanga nauli mbalimbali, Mamlaka inazingatia vifungu namba 5 (1) (c) (iii) na 21 (2) (b) vya Sheria ya LATRA Na. 3 ya Mwaka 2019 pamoja na Kanuni ya 15 ya Tozo za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini ya Mwaka 2020, GN. Na. 82 ambavyo vimeelekeza kuzingatia mambo yafuatayo;

 1. Gharama za utoaji huduma za usafiri wa mabasi
 2. Nauli shindanishi kwenye soko
 3. Kulinganisha nauli na mahali pengine na faida ya utoaji huduma
 4. Maslahi ya Walaji (abiria) na watoa huduma za usafiri wa mabasi
 5. Kulinda mitaji ya wawekezaji pamoja na;
 6. Maoni ya wadau

Hivyo basi maoni ya wadau ni muhimu sana katika kufanikisha upangaji wa nauli muda utakapowadia.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Kwa hayo machache, napenda kukukaribisha uongee na hadhara hii kisha utufungulie mkutano wetu.

Asanteni kwa kunisikiliza

Gilliard W. Ngewe

Mkurugenzi Mkuu

26 Mei, 2022

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo